Sunday, August 30, 2009

MWEZI WA RAMADHAN: Bei za Vyakula wala hazijapanda kiviiile..

Si ajabu kukuta watu wakilalamikia kuhusu kupanda kwa bei za vyakula kila unapofika mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ukiuliza wafanyabiashara kwa nini bei za vyakula hasa vile vya futari kama ndizi, mihogo, viazi, maharage na vinginevyo vinapanda bei, watakwambia gharama za usafirishaji zipo juu.

Wengine watakwambia wakulima wenyewe ndio wanaopandisha bei za mazao huko mashambani. Lakini kwa ujumla ukiangalia harakaharaka utagundua kuwa imekuwa ni kama 'fasheni' kwao kufanya hivyo kwa misingi ya ki'maslahi' yao binafsi.

Wanajua kuwa hata ufanyeje lazima tu utanunua mihogo ama ndizi kwa ajili ya kwenda kutengeneza futari, hivyo huna njia ya kukwepa... Lakini hili linawezekana kukemewa na kusimamiwa ipasavyo na Mamlaka za masoko na hali ikawa shwari kabisa.

Ukiliangalia suala hili kwa misingi ya kimatabaka, utagundua kuwa tabaka la watu fulani ndilo linaloathirika zaidi na upandishwaji wa bei za vyakula hivi, wakati tabaka fulani haliathiriki kutokana na tofauti ya vipato.

Tuachane na hilo, lakini jana nilitembelea katika masoko mawili maarufu kwa vyakula hivi, soko la Temeke Stereo na la Buguruni, hali nilikuta tofauti. Kwa kweli bei za vyakula hazikuwa za kutisha zilikuwa ni za kawaida tu, mfano fungu moja la mihogo lilikuwa ni kati ya sh 500 na 1000, wakati ndizi moja ya mzuzu iliuzwa kati ya 200 na 250 bei ambazo ni za siku zote.

Niliwauliza wafanyabiashara kuwa kwa nini wakati watu wanalalamika huko mitaani kuwa bei za vyakula zipo juu , hali ni tofauti katika masoko hayo walinijibu kuwa, tatizo hawatembelei masokoni na badala yake wanatembelea kwenye magenge na ndo maana wanalalamika kuwa bei za vyakula zimepanda.

Nikagundua kuwa, alaa kumbe watu hawana utamaduni wa kutembelea masoko kama haya na kuishia kulalamikia kupanda kwa bei za vyakula... jamani tutembeleeni masoko yetu ili tukanunue bidhaa zetu kwa bei nafuu..



Wafanyabiashara za ndizi wakiwajibika sokoni Buguruni


Wananchi wakinunua mihogo sokoni Buguruni

No comments:

Post a Comment