Monday, August 2, 2010

MTIKILA AYEYA JELA MIEZI 6

Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha DP amedakwa leo na makachero waliokuwa wakimsaka muda mrefu huku wakiwa na 'kibali cha kumkamata' na kufikishwa Mahakama ya wilaya Ilala ambako alikuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita hapo awali.

Mtikila ambaye alionekana kutoamini jambo hilo huku akionekana mwenye kujiamini zaidi, alikuwa akidaiwa deni la zaidi ya shilingi milioni 9 na mkazi mmoja wa jijini hapa Dar es Salaam, Mama Pascazia Zelamula Matete (61) ambaye kitaaluma ni Mwalimu.

Kwa mujibu wa Mama Pascazia, alimkopesha fedha hizo ili ziweze kumsaidia kwenye biashara zake, lakini imekuwa ngumu kwa Mtikila kurudisha fedha hizo kiasi cha kumsababishia mama huyo kutengwa na familia yake hususan mumewe ambaye alimwambia atamrudia tu endapo atakuwa amerudishiwa fedha hizo.


Mtikila akiingia kwenye gari la Polisi kuelekea kituo cha Msimbazi leo

"Hata watoto wangu nao wamenitenga, sasa naishi maisha magumu, nimetengwa na mume wangu, watoto wangu sababu ya huruma yangu ya kumsaidia Mtikila. Leo siondoki hapa, nitafia hapahapa mpaka fedha zangu azirudishe." Alisema mama huyo.

Mtikila alichukuliwa na gari la Polisi wa Kituo cha Msimbazi na kupelekwa kituoni huko kwa ajili ya kuhifadhiwa bada ya muda wa mahakama kuwa umekwisha na anatarajiwa kupelekwa jela kwa kipindi cha miezi sita, jambo ambalo binafsi ameridhia.

No comments:

Post a Comment