Kampuni ya kuhudumia makontena bandarini (TICTS) jana imetimiza miaka 10 tangu kuanza kutoa huduma zake hapa nchini huku ikiwa imebadilisha taswira ya awali iliyokuwepo kwenye bandari zetu nchini.
Waziri wa Miundombinu Dk Shukuru Kawambwa anasema kuwa hali ya upakuaji makontena kwenye bandari zetu kabla kampuni hiyo haijaanza kuendesha shughuli zake hapa nchini ilikuwa si yakuridhisha ukilinganisha na sasa. "Tunaiombea iendelee kuleta mabadiliko mpaka kufikia mwaka 2025." Alisema.
Katika kuhakikisha shughuli za upakuaji makontena kwenye bandari zetu zinaboreshwa, jana kampuni hii imezindua winchi mpya moja yenye kasi na uwezo wa kubeba makontena mawili kwa wakati mmoja na kufanya idadi ya winchi nne yaani 'cranes'.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TICTS, Neville Bissett amewaambia waandishi wa habari pamoja na wadau waliohudhuria hafla hiyo jana Dar es Salaam kuwa kampuni yake kwa kushirikiana na vitengo mbalimbali vinavyotoa huduma bandarini hapo ikiwemo TRA, inaendelea kuboresha utendaji kazi wake ili kumaliza kabisa tatizo la mlundikano wa makontena.
Amewatoa hofu wateja wanaotumia bandari hiyo na kuwahakikishia mabadiliko ya hali ya juu zaidi. "Tumeboresha shughuli zetu ukilinganisha na tulivyoanza. Uwezo wetu umekuwa mkubwa kwa kuongeza winchi mpya na za kisasa zaidi." Alisema.
No comments:
Post a Comment