Sunday, October 31, 2010

ZAIDI YA NUSU YA WATANZANIA WALIOJIANDIKISHA HAWAJAPIGA KURA, WAANGALIZI WA SADC WASEMA HALI NI MBAYA, WAIOMBA SERIKALI KUNUSURU

Zaidi ya nusu ya watanzania waliojiandikisha kwenye daftari la kupiga kura hawakujitokeza kwenye zoezi la upigaji kura lililofanyika leo, kwenye maeneo mbalimba ya nchi.


Wasimamizi wakisubiri wapigakura

Wilaya ya Mkuranga, zaidi ya vituo vitano mahudhurio yalikuwa hayafikii hata nusu ya malengo. Katika kituo cha Godown-3, idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa ni 465 lakini mpaka kufikia saa saba mchana ni wapigakura 122 tu ndiyo waliojitokeza kupiga kura.

Kwenye kituo cha Shule ya Msingi Kiguza, mategemeo yalikuwa ni wapigakura 254, lakini mpaka kufikia saa sita mchana ni wapigakura 111 tu ndiyo waliojitokeza kupiga kura, hata hivyo hakukuwa na dalili yoyote ya kufikia alau nusu ya malengo hayo kutokana na mahudhurio ya mtu mmoja mmoja zaidi ya hata robo saa.

"Labda watakuja baadaye, asubuhi kunzia saa moja mpaka saa tatu ilikuwepo misururu mirefu, lakini kama unavyoona sasa hivi tumejikalia tu tunasubiri labda watakuja kabla ya saa 10." Alisema Msimamizi wa Kituo hicho, Malik Mporau.


Mawakala wakihakiki karatasi za kura

Hali ilikuwa ni hivyo kwenye kituo cha Picha ya Ndege-3 safari hii ikiwa mbaya zaidi, ambapo katika wananchi 400 waliolengwa kupiga kura, waliojitokeza ni 80 tu mpaka kufikia saa saba na nusu.

Katika Kata ya Toangoma, Kigamboni kwenye kituo cha Kongowe C-4, malengo yalikuwa ni wapigakura 420, lakini idadi iliyojitokeza ni wapigakura 120 tu mpaka kufikia saa nane mchana. Halikadhalika kwenye Jimbo la Mbagala, Kituo cha Ofisi ya Tarafa-3, waliokuwa wameandikishwa kwenye daftari la kupigia kura walikuwa ni 449 lakini waliojitokeza kupigakura mpaka saa nane na robo (saa moja na nusu baadaye kufungwa kwa zoezi) mchana walikuwa ni 130.

Napo kwenye kituo cha Bustani 4, Kata ya Mtoni ni watu 490 walioandikishwa kwenye daftari la kupiga kura, lakini mpaka kufikia saa tisa ni wapigakura 150 tu ndiyo waliokuwa wamejitokeza kupiga kura, kwa mujibu wa Radhia Hassan.

Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), na wale wa kutoka Jumuiya ya Madola (Common Wealth) walionesha kushtushwa na hali hiyo na kuishauri Serikali kuliangalia hilo kwa kuwashawishi wananchi wake kujitokeza kupiga kura kwenye chaguzi zijazo.

Mmoja wa wakala wa uchaguzi aliyefahamika kwa jina la Suleiman Iddi alisema kuwa waangalizi hao walitoa ushauri huo baada ya kubaini kuwa hali haikuwa shwari.

No comments:

Post a Comment