Monday, February 7, 2011

WANAFUNZI UDSM WAPIGWA MABOMU YA MACHOZI WAKIDAI SH 10,000 YA 'BOOM'

Askari wa kutuliza ghasia 'ffu' leo mchana wamewavurumishia mabomu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuisha kwa mkutano wao na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa uliokuwa ukijadili ongezeko la kiwango cha fedha za kujikimu 'Boom' kwa wanafunzi hao.

Muda mfupi baada ya kuondoka kwa waziri huyo, wanafunzi hao walianza kuwaandama askari hao waliokuwa wakiondoka eneo hilo kwa kuwarushia mawe, chupa za maji na vitu vinginevyo, na kuwazomea jambo ambalo lilizua tafrani kubwa baina ya askari na wanafunzi hao na kulazimika kufyatua mabomu ya machozi kwa mfululizo kwa wanafunzi hao waliokuwa wakivurumisha mawe kwa mfululizo.

Hata hivyo askari hao walifanikiwa kutawanya maelfu ya wanafunzi hao waliokuwa wakiwazonga askari hao waliokuwa na magari maalumu aina ya Defender na Land Cruiser, na kuacha wengine wakiwa wamezimia na wengine kujeruhiwa na mabomu hayo.

Awali katika mkutano wao wanafunzi hao na waziri Kawambwa, walimtaka waziri huyo atoe tamko la ongezeko la kiwango cha fedha hizo kutoka shilingi 5,000 ya sasa mpaka 10,000 waliyokuwa wakidai, jambo ambalo lilimpa wakati mgumu waziri huo kulitolea uamuzi wa moja kwa moja, ambapo kila alipokuwa akizungumzia 'mchakato' wanafunzi hao walikuwa wakizomea na kusema "Hatutaki siasa, tunataka elfu kumi tu."

Hata hivyo Waziri Kawambwa alilazimika kuahirisha mkutano huo baada ya hali kuanza kuwa tete pale wanafunzi hao walipoanza kufanya fujo huku wakimlazimisha atoe tamko litakalowaridhisha wanafunzi hao. "Mimi nimewasikia, nitaenda kushauriana na Hazina tuone namna gani tunaongeza kiwango hcho, lakini si elfu kumi kama mnavyodai.." Alisema hivyo waziri Kawambwa na kusababisha maelfu ya wanafunzi hao waliokuwa wakimsikiliza kuanza kupiga kelele kwa kusema "tunatakaa, aashuukee... Tunataakaa, aashuukee..." na ndipo waziri kawambwa alipoufunga mkutano huo na kuondoka huku akiwaacha wanafunzi hao wakiwa na maswali mengi ya kujiuliza.

Muda mfupi baada ya waziri Kawambwa kuondoka eneo hilo, wanafunzi hao walihamishia hasira zao kwa askari wa kutuliza ghasia 'ffu' kwa kuanza kuwavurumishia mawe, chupa za maji na vitu vingine huku wakiwazomea, jambo lililopelekea askari hao kuanza kufyatua mabomu ya machozi kwa mfululizo na kupelekea eneo hilo kugeuka na kuwa la vita, huku vishindo vikubwa vya mabomu hayo vikisikika na kusababisha moshi mwingi kutanda angani.

HABARI PICHANI:









No comments:

Post a Comment