Nilipokaribia eneo hilo ambalo ni kambi ya Magereza ya Ukonga, nilistaajabu kuona misitu ya asili iliyoshibana na kupelekea hewa safi kuzunguka eneo. Baada ya kushuka garini Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Magereza, Menrad Tesha alitutembeza kuangalia baadhi ya vivutio vya asili vilivyomo katika eneo hilo.
"Kwa ujumla eneo lote la hifadhi lina ukubwa wa ekari 1000." Alianza kwa kusema ACP Tesha na kuendelea, "Eneo hili linapakana na hifadhi ya wanyama ya Selous, upande wa Kusini Mashariki pamoja na Kijiji cha Kiboga." Alisema.
Baadaye tukafika eneo ambalo kuna msitu pamoja na kuweka vichaka vilivyofungamana ambalo kwa mujibu wa Kamanda Tesha alisema ni makazi ya Tembo. "Si tembo tu, wakati mwingine unaweza kuwaona Simba, Duma, Swala na Chui." Alisema. Nilishangazwa zaidi tulipofika katika bwawa la matope la kuhifadhi viboko. Duh, nilistaajabu kweli haki ya Mungu.
bwawa hilo ambalo juu yake kumestawi majani ama magugu yanayohifadhi maji ni kubwa kweli ambalo unaweza kulilinganisha na lile la Mindu kule Morogoro. Nilijaribu kudodosa kidogo kutaka kufahamu historia ya hilo bwawa, nikaambiwa kuwa hapo awali kulikuwa na kijiji fulani hivi kabla ya kuzama na kutengeneza bwawa hilo.
Baadaye tulipomaliza kuzungukia maeneo hayo mbalimbali, tukajipumzisha mahali kupata madafu na machungwa. Kwa kweli nilivutiwa sana na eneo hilo kwa ujumla. Nikagundua kuwa, unaweza kufanya utalii wa kutosha eneo hilo badala ya kwenda mbali na nje ya jiji hili.
Hiyo ndiyo Hifadhi ya Kambi ya Magereza ya Ukonga, iliyopo eneo la Mvuti, wilayani Ilala jijini hapa ambayo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali tulifanya ziara kuangalia vivutio vya kitalii mwishoni mwa wiki iliyopita.
waandishi wa habari wakipenya katika moja ya miti iliyofungana katika hifadhi hiyo..
waandishi wa habari wakipenya katika moja ya vichaka vya hifadhi hiyo..
Moja ya kisima chenye historia kubwa ya hifadhi hiyo...
ACP Menrad Tesha (kushoto) akiwaongoza baadhi ya waandishi wa habari na maofisa wa Magereza kuangalia bwawa la matope linalohifadhi viboko hifadhini hapo...
No comments:
Post a Comment