Thursday, February 4, 2010

JK ATAKA MAHAKAMA KUHARAKISHA UTOAJI HUKUMU

Rais Jakaya Kikwete amezitaka Mahakama nchini kurekebisha kasoro zinazolalamikiwa na wananchi ambazo zinatia doa mwenendo wa utoaji haki nchini.

Rais Kikwete alisema hayo wakati akihutubia jopo la Majaji wakuu wa Mahakama, Mawakili na Wanasheria wakati wa maadhimisho ya siku ya Sheria nchini yaliyofanyika leo asubuhi katika eneo la Mahakama Kuu, jijini hapa.

"Bado kuna malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa usikilizaji kesi na utoaji hukumu pia. Aidha, kuna malalamiko kuhusu kuchelewa kuandikwa kwa hukumu na kuna kilio cha baadhi ya watumishi wa mahakama kuomba na kupokea rushwa," Alisema na kuendelea,

"Kasoro hizo zinatia doa katika mwenendo mzima wa utoaji haki nchini. Hamna budi kufanya kila iwezekanavyo kuziondoa kasoro hizo. Naamini inawezekana. Naamini mnaweza. Yes you can," Akaendelea tena,

"Nafurahi kwamba wenyewe mnatambua hizo kasoro na mnachukua hatua kuzirekebisha." Alisema Rais Kikwete.



Hata hivyo Rais Kikwete amewasifu Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa kitendo alichokiita cha Kizalendo zaidi cha kuacha kwenda kula Sikukuu za mwisho wa mwaka jana, badala yake kufanya Kikao kwa ajili ya kumalizia mashauri takribani 82 ambayo hata hivyo ni Mashauri 61 kati ya hayo ambayo yamesikilizwa na yanayosuburi kutolewa Maamuzi ni 8.

"Nimefurahishwa sana na kitendo cha kizalendo, niliposikia kwamba Majaji wa Mahakama ya Rufani, waliacha kwenda kwenye mapumziko ya “Chrismas Vacation” ya mwaka jana, mapumziko ambayo hufanyika kila mwezi wa Disemba mpaka Januari, badala yake wamekaa na kufanya kikao maalum (special session) ambacho kimemalizika tarehe 29/01/2010" Alisema.

No comments:

Post a Comment