Friday, March 26, 2010

AJALI YA KIBAMBA: MAMA MJAMZITO, BABA NA MTOTO WAFA, NI SIMANZI MITAA YA KIBAMBA

Katika hali ya kusikitisha imebainika kuwa Baba, Mama na Mtoto ni miongoni mwa waliokufa katika ajali ya gari iliyotokea Kibamba Darajani, Dar es Salaam jana.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Sponsor leo katika mitaa mbalimbali ya Kibamba, imebainika kuwa marehemu Ibrahim Hussein na mke wake Zainab Ally ambaye alikuwa ni mjamzito walikufa papo hapo katika ajali hiyo wakiwa njiani kuelekea hospitali.

Mdogo wa Marehemu Zainab, Sharifa Ally ameiambia Sponsor kuwa marehemu hao mume na mke wake ambaye alikuwa ni mjamzito iliwalazimu kuondoka mapema alfajiri kuelekea hospitali ili kuepuka misururu ya magari iliyozoeleka katika barabara ya Morogoro, lakini hawakufikia malengo yao na ndipo umauti ulipowakuta njiani, meta chache sana kutoka walipopandia daladala. Marehemu Zainab alikuwa katika hatua za mwisho za kujifungua.

Katika ajali hiyo ya kusikitisha, ujauzito wa marehemu Zainab uliharibika vibaya palepale na mtoto kutoka nje kwa bahati mbaya. Kwa maana nyingine tunaweza kusema, marehemu Zainab alijifungua kwa lazima na tena kwa njia isiyo halali.

Miili ya marehemu hao wote watatu inatarajiwa kuzikwa jioni hii katika makabauri yaliyopo jirani na nyumbani kwao, Kibamba Dar es Salaam. Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.


Mtoto Mwanaidi Ibrahimu, yatima aliyeachwa na wazazi wake wawili

Katika hatua nyingine, Sponsor imeshuhudia simanzi iliyotawala katika mitaa mbalimbali ya Kibamba CCM ambako asilimia kubwa ya abiria waliokufa katika ajali ile waliokuwa wakiishi huko.

Haikuwa rahisi kutoona vikundi vya watu vikijadili hili na lile kuhusiana na tukio lile la ajali ya Kibamba.

Nyumbani kwa Mzee Hussein, ambaye kijana wake ndie aliyekuwa kondakta wa daladala lile napo vilio na simanzi vilitawala.

"Tunasafirisha leo kwenda kuzika kwa Ngwandu, Tanga." Alisema mzee Hussein.


Ndugu wa karibu wakiomboleza msiba wa marehemu Shukuru Hussein, aliyekuwa kondakta wa daladala iliyopata ajali

No comments:

Post a Comment