Tuesday, November 16, 2010

PINDA NDIYE WAZIRI MKUU


Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amemtangaza Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano iliyobaki.

Spika Makinda alimtaja Mheshimiwa Pinda kuwa Waziri Mkuu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kupitia waraka wake aliomuandikia spika huyo na kusomwa mbele ya wabunge wa bunge hilo leo jioni.

"Nachukua fursa hii kumtangaza Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania." Alisema spika Makinda wakati akisoma barua hiyo iliyotumwa kwake.

Monday, November 15, 2010

WANAJESHI WA UINGEREZA WATOA MAFUNZO YA KUPAMBANA NA MAHARAMIA KWA WANAJESHI WA TANZANIA

Askari wa Jeshi la wanamaji wa Uingereza wamo nchini kwa siku tano ambapo wataendesha mafunzo ya kijeshi kwa askari wa jeshi la wanamaji hapa nchini ya namna ya kupambana na maharamia.

Askari hao waliowasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kwa meli ya kivita ya HMS Montrose watakuwepo kwa siku tano kabla ya kuondoka, ambapo vikosi mbalimbali vya wanamaji wa Tanzania vitapewa mbinu na mafunzo ya namna ya kupambana na maharamia.

Wakiwa njiani kuja hapa nchini, askari hao wameweza kudhibiti maharamia wa somalia kwa kiwango kikubwa. Kamanda wa meli hiyo, Jonathan Lett anasema, "Tumeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa maharamia katika pwani ya Somalia." Alisema.



British Royal Navy soldier, Rob McMurrich with his General Purpose Machine Gun

Sunday, November 7, 2010

MAJERUHI CHENGE ATANGAZA KUGOMBEA USPIKA



Mbunge mteule wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ametangaza azma yake ya kugombea bafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Dar es Salaam.

Chenge ametangaza azma yake hiyo mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini alipofanya nao mkutano kwenye hoteli ya Courtyard, eneo la Upanga Sea view, majira ya saa sita mchana.

"Nimewaita hapa leo ndugu zangu kwa lengo moja tu la kutangaza azma yangu ya kugombea nafasi ya Uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili niweze kutibu majeraha makubwa yaliyoumiza Bunge, Taifa na wananchi wa chama changu (CCM). Mimi kama ilivyo kwa wengine ni miongoni mwa majeruhi wa uongozi, Kama bunge, hatuna budi kukabiliana nalo kwa nguvu kubwa." alisema na kuongeza,

"Bunge letu limekuwa na changamoto kubwa katika miaka mitano iliyopita. Viongozi ambao wajibu wetu ni kuonesha njia badala yake tumekuwa vinara wa uzushi, uongo, fitna na majungu. Mimi ni mwarobaini (dawa ya kutibu) wa majeraha hayo, ambaye naamini ni kiongozi bora na nina uwezo na nia thabiti." Alisema