Monday, July 13, 2009

Mdau katika pingu za maisha





Nilikuwa nahesabu miezi, ikawa masiku sasa na hatimaye yakabaki masaa, mwishowe zikabaki dakika na sekunde... ilipotimu saa mbili za usiku baada ya swala ya ishaa mambo yakawekwa hadharani... Sheikh aliniambia nimshike mkono baba mkwe na tendo la kufunga ndoa likawadia... "Mimi Fadhili bin Akida, namuoa Shufaa binti Kombo Sweid kwa mahari tuliyokubaliana..." Sheikh ndiye aliyekuwa akitamka maneno hayo na kuniambia nami niyatamke... ikawa hivyo na maneno mengine na punde mambo yakawa yamekamilika.

Bila shaka nimeoa... Sasa siyo tena 'bachela' kama mama zangu wadogo walivyozoea kunitania hapo awali... Sasa siyo tena 'muhuni' kama baba yangu mdogo 'Seif Luwinzo' alivyozoea kunitania hapo awali... Sasa sitokawia tena kurudi nyumbani usiku wa manane kama ilivyokuwa hapo awali... Hakika nimeyaanza maisha mapya kabisa ambayo nilikuwa nikiyatamani wakati wa utoto wangu... Nilipokuwa mtoto nilitamani siku moja na mimi niwe mkubwa na kisha kuitwa baba kama nilivyokuwa namwita baba yangu enzi za utoto wangu... Hii ni hali ya kawaida ambayo wengi wenu mlishaipitia mkiwa watoto.

Fungate limekwisha sasa nimerudi kazini nawajibika huku nikiwa na fikra za nyumbani kwa mke wangu... Namuwaza mke wangu, nafikiria leo atapika nini... wakati mwezi mmoja kabla siku kama ya leo sikuwa na fikra hizi... ama kweli mambo yanakwenda yakibadilika... na siku hazigandi... ah!

Rafiki zangu na wafanyakazi wenzangu wananipa hongera nimeoa... Ahsante Mungu na namuomba anipe maisha mazuri ya ndoa na mke wangu... atuepushe na mabalaa... atufungulie milango ya neema... Amin!

Karibuni tena wasomaji wangu katika blog hii... mambo yanaendelea kama kawaida... utahabarika zaidi ya hapo awali...

No comments:

Post a Comment