Sunday, October 31, 2010

BURIANI ELVIS MUSIBA



Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA), Elvis Musiba amefariki dunia leo kwenye hospitali ya TMJ, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ndugu wa familia hiyo, marehemu Musiba alikutwa na mauti hayo majira ya saa nne asubuhi hospitalini hapo kutokana na maradhi ya mguu yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

Marehemu Musiba alikuwa akisumbuliwa na maradhi hayo ambapo mwezi oktoba mwaka huu alipelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kabla ya kufikishwa hospitalini hapo Jumamosi ya wiki iliyopita kwa mujibu wa ndugu hao.

Taratibu za mazishi zinafanywa nyumbani kwa marehemu Mikocheni, Dar es Salaam.

Marehemu Musiba katika uhai wake aliwahi kuwa Mtunzi mashuhuri wa simulizi za riwaya ambazo ni pamoja na 'Kufa na Kupona, Kikomo, Kikosi cha Kisasi, Njama na Hujuma na nyinginezo ambapo pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali za wakurugenzi zikiwemo Sematel Ltd (DRC), Exclusive Lodges Resort Ltd, Kamati ya Mahesabu ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Akaunti ya Milenia (Tanzania) na Kituo cha Uwekezaji cha TIC.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali pema Peponi, Amina.

ZAIDI YA NUSU YA WATANZANIA WALIOJIANDIKISHA HAWAJAPIGA KURA, WAANGALIZI WA SADC WASEMA HALI NI MBAYA, WAIOMBA SERIKALI KUNUSURU

Zaidi ya nusu ya watanzania waliojiandikisha kwenye daftari la kupiga kura hawakujitokeza kwenye zoezi la upigaji kura lililofanyika leo, kwenye maeneo mbalimba ya nchi.


Wasimamizi wakisubiri wapigakura

Wilaya ya Mkuranga, zaidi ya vituo vitano mahudhurio yalikuwa hayafikii hata nusu ya malengo. Katika kituo cha Godown-3, idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa ni 465 lakini mpaka kufikia saa saba mchana ni wapigakura 122 tu ndiyo waliojitokeza kupiga kura.

Kwenye kituo cha Shule ya Msingi Kiguza, mategemeo yalikuwa ni wapigakura 254, lakini mpaka kufikia saa sita mchana ni wapigakura 111 tu ndiyo waliojitokeza kupiga kura, hata hivyo hakukuwa na dalili yoyote ya kufikia alau nusu ya malengo hayo kutokana na mahudhurio ya mtu mmoja mmoja zaidi ya hata robo saa.

"Labda watakuja baadaye, asubuhi kunzia saa moja mpaka saa tatu ilikuwepo misururu mirefu, lakini kama unavyoona sasa hivi tumejikalia tu tunasubiri labda watakuja kabla ya saa 10." Alisema Msimamizi wa Kituo hicho, Malik Mporau.


Mawakala wakihakiki karatasi za kura

Hali ilikuwa ni hivyo kwenye kituo cha Picha ya Ndege-3 safari hii ikiwa mbaya zaidi, ambapo katika wananchi 400 waliolengwa kupiga kura, waliojitokeza ni 80 tu mpaka kufikia saa saba na nusu.

Katika Kata ya Toangoma, Kigamboni kwenye kituo cha Kongowe C-4, malengo yalikuwa ni wapigakura 420, lakini idadi iliyojitokeza ni wapigakura 120 tu mpaka kufikia saa nane mchana. Halikadhalika kwenye Jimbo la Mbagala, Kituo cha Ofisi ya Tarafa-3, waliokuwa wameandikishwa kwenye daftari la kupigia kura walikuwa ni 449 lakini waliojitokeza kupigakura mpaka saa nane na robo (saa moja na nusu baadaye kufungwa kwa zoezi) mchana walikuwa ni 130.

Napo kwenye kituo cha Bustani 4, Kata ya Mtoni ni watu 490 walioandikishwa kwenye daftari la kupiga kura, lakini mpaka kufikia saa tisa ni wapigakura 150 tu ndiyo waliokuwa wamejitokeza kupiga kura, kwa mujibu wa Radhia Hassan.

Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), na wale wa kutoka Jumuiya ya Madola (Common Wealth) walionesha kushtushwa na hali hiyo na kuishauri Serikali kuliangalia hilo kwa kuwashawishi wananchi wake kujitokeza kupiga kura kwenye chaguzi zijazo.

Mmoja wa wakala wa uchaguzi aliyefahamika kwa jina la Suleiman Iddi alisema kuwa waangalizi hao walitoa ushauri huo baada ya kubaini kuwa hali haikuwa shwari.

Friday, October 29, 2010

SIGARA HATARI!



Ni dhambi kubwa kwa Mungu kwa mtu anayejitoa mwenyewe uhai wake kwa namna yeyote ile. Unapofanya jambo ambalo unafahamu kuwa mwisho wa siku litakutoa uhai, ni sawa na kujinyonga mwenyewe.

Pichani ni pakiti za sigara zenye onyo kali kwa wavutaji wake. Ajabu ni kwamba onyo hilo limechukua nafasi kubwa kuliko nembo yenyewe ya bidhaa hiyo. Je, kwa hali hii,ukifa nani wa kulaumiwa wakati ushapewa onyo tena kwa maandishi makubwa tu?

DINI-VIONGOZI WA DINI WAUSIA UCHAGUZI WA AMANI

Viongozi wa dini leo wamefanya ziara kwenye vyama mbalimbali vya siasa kuhimiza Uchaguzi wa amani nchini.

Wakiwa kwenye Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), viongozi hao wamesisitiza uchaguzi wa haki ili wananchi wawapate wale viongozi waliowachagua na si vinginevyo.



"Hata vitabu vya dini vinakemea dhuluma ya haki, kila mwana adamu ana haki ya kuchagua akipendacho." Alisema Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum.



Naye Askofu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini (TEC), Paul Rukoza amesema kuwa wananchi wanatakiwa kujifunza ustahamilivu wakati wakupokea matokeo. Amesema kuwa wakati wa kmapeni kila upande hujiamini kupita kawaida kutokana na maandalizi jambo ambalo mwisho wa siku huweza kuibua malumbano na machafuko na kuathiri mfumo wa maisha.

"Hata hivyo tunapenda kuviasa baadhi ya vyombo vya habari vyenye mitazamo hasi kuhusu mikutano yetu sisi viongozi wa dini." Alisema

BEACH ZETU CHAFU!!

Huu ni ufukwe na wala si dampo. Eneo hili ni maarufu sana hapa mjini ambalo mwisho wa wiki wananchi hupendelea kwenda kujipumzisha na wengine kuoga kwa ajili ya kupunguza joto la jiji hili.



Eneo hili ni Ufukwe wa Coco almaarufu 'Coco Beach'. Lakini mandhari inayoonekana hapa haivutii kutokana na taka bahari zilizolundikana.

Je, kwa hali hii kuna ulazima wa kuendelea kuwapigia kelele wawekezaji wa kigeni kuwa wanatunyima wazalendo fursa za kufanya biashara? Mfano ufukwe huu ungekuwa chini ya mwekezaji wa kigeni unadhani hali ingekuwaje?

Tufanye kazi watanzania wenzangu na tuache kubweteka kwani mafanikio hayaji kiurahisi rahisi tu!

MATUNDA BWERERE, WAPI VIWANDA?

Tanzania imejaaliwa kwa kuwa na ardhi yenye kukubali kila aina ya zao. Matunda ni miongoni mwa mazao yanayostawi vizuri kwenye ardhi ya nchi hii. Unapofika msimu wake, matunda huwa ni mengi sana kwenye masoko yetu 'local markets'.

Huruma huwa inanijia pale ninapoona matunda hayo yanapokuwa mengi kwenye masoko yetu na kukosa wanunuzi ambapo mwisho wa siku huwa yanaoza, kuharibika kabisa mikononi mwa wafanyabiashara.



Wapi viwanda vya usindikaji wa matunda haya? Wapi viwanda vya kutengeneza 'juisi' za matunda haya? Matunda kama Machungwa, Maembe, Mananasi na mengineyo?

Kwanini Kenya waweze, sisi tushindwe? Kwa nini? Mchawi ni nani? Ona pichani ndizi hizi mbivu kwenye Soko la Buguruni zilivyolundikana hapo chini zikitafuta wanunuzi!! Baada ya siku chache pita tena hapohapo sokoni utaona namna ndizi hizo zilivyo ozeana, kulaliana na kupondekapondeka!