Monday, August 9, 2010

HONGERA FAHIM! MIEZI MITANO SI MIDOGO!!



Zilikuwa Siku, Wiki na sasa ni Miezi mitano tangu ulipozaliwa,
Mungu akupe uhai, ufike mbali ukubwani, Maisha ni Mitihani,
Hongera Fahim mwanangu, Miezi Mitano umeitimiza!

HAPA NDIPO ANAPOANDALIWA PWEZA?



Mkazi huyu wa jijini Dar es Salaam alikutwa na blogu hii akiandaa samaki aina ya pweza na ngisi kwenye mazingira machafu leo asubuhi, Soko la Samaki Magogoni (Feri). Maandalizi ya chakula kwenye mazingira ya aina hii ni hatari hasa ukuzingatia mtumiaji ni binadamu mimi na wewe.

Mamlaka zinazohusika na masuala ya usafi wa mazingira kwenye maeneo nyeti hasa Sokoni hazina budi kuchukua tahadhari kwa kufanya ziara za mara kwa mara maeneo hayo kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata taratibu na kanuni za usafi wakati wakiandaa bidhaa zao ili kuepusha maradhi ya milipuko kwa watumiaji.

Friday, August 6, 2010

WAZIRI LI DONGDONG WA CHINA ATEMBELEA TSN



Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya TSN inayochapisha magazeti ya Serikali ya Daily News na Habari Leo, Mkumbwa Ally (kushoto) akimtembeza mgeni wake, Naibu Waziri wa Uchapishaji na Habari wa China, Bi. Li Dongdong kuangalia shughuli za uzalishaji wa magazeti hayo ndani ya ofisi za Kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam leo asubuhi. [Picha: kwa hisani ya Yusuf Badi wa TSN]

SHEIN AFUNGUA UJENZI KITUO CHA AFYA BUMBWI SUDI



Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Wananchi wa kijiji cha Bumbwi Sudi kiliopo katika Wilaya ya Magharibi Unguja leo. jumla ya shilingi miloni 25.4 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho. [Picha: Kwa hisani ya Amour Nassor wa VPO]

KITI CHA KWANZA CHA SPIKA WA BUNGE LA TANGANYIKA LA MWAKA 1962


Hiki ndo' kiti cha kwanza cha Spika wa Bunge ambacho kilitolewa kama zawadi na Bunge la  Uingereza (House of Common) kwa Bunge la Tanganyika mwaka 1962 mara baada ya Uhuru. Kiti hiki kimetumika nchini mpaka mwaka 2005. [Picha: kwa hisani ya Owen Mwandumbya wa Bunge].

Monday, August 2, 2010

MTIKILA AYEYA JELA MIEZI 6

Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha DP amedakwa leo na makachero waliokuwa wakimsaka muda mrefu huku wakiwa na 'kibali cha kumkamata' na kufikishwa Mahakama ya wilaya Ilala ambako alikuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita hapo awali.

Mtikila ambaye alionekana kutoamini jambo hilo huku akionekana mwenye kujiamini zaidi, alikuwa akidaiwa deni la zaidi ya shilingi milioni 9 na mkazi mmoja wa jijini hapa Dar es Salaam, Mama Pascazia Zelamula Matete (61) ambaye kitaaluma ni Mwalimu.

Kwa mujibu wa Mama Pascazia, alimkopesha fedha hizo ili ziweze kumsaidia kwenye biashara zake, lakini imekuwa ngumu kwa Mtikila kurudisha fedha hizo kiasi cha kumsababishia mama huyo kutengwa na familia yake hususan mumewe ambaye alimwambia atamrudia tu endapo atakuwa amerudishiwa fedha hizo.


Mtikila akiingia kwenye gari la Polisi kuelekea kituo cha Msimbazi leo

"Hata watoto wangu nao wamenitenga, sasa naishi maisha magumu, nimetengwa na mume wangu, watoto wangu sababu ya huruma yangu ya kumsaidia Mtikila. Leo siondoki hapa, nitafia hapahapa mpaka fedha zangu azirudishe." Alisema mama huyo.

Mtikila alichukuliwa na gari la Polisi wa Kituo cha Msimbazi na kupelekwa kituoni huko kwa ajili ya kuhifadhiwa bada ya muda wa mahakama kuwa umekwisha na anatarajiwa kupelekwa jela kwa kipindi cha miezi sita, jambo ambalo binafsi ameridhia.

Sunday, August 1, 2010

KURA ZA MAONI ZANOGA: MTEMVU AONGOZA KATA YA MTONI: JANGWANI NUSURA ZICHAPWE KAVUKAVU: KADI FEKI ZAKAMATWA

Zoezi la upigaji kura za maoni kwa wanachama wa CCM kwenye matawi mbalimbali jijini hapa limekuwa na sura mbalimbali ambapo Jimbo la Temeke, Mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo Abbas Mtemvu mpaka kufikia majira ya saa moja usiku alikuwa akiongoza kwa kura Kata ya Mtoni.

Vituko vilianza kuibuka kwenye matawi mbalimbali huku kukiwa na malalamiko kadhaa kwa wanachama kuzuiliwa kupiga kura kutokana na majina yao kutoorodheshwa kwenye rejista mpya. Tawi la Misewe, Darajani na Segerea yote yakiwa kwenye Jimbo la Segerea malalamiko yalikuwa ya aina hiyo.



Jangwani, vituko vya kubiduliwa biduliwa kwa masanduku ya kupigia kura vilileta sura tofauti kabisa. Sababu inadaiwa ni kuwa majina ya watu yalikutwa yamepewa tiki kwenye rejesta ya majina.

Halikadhalika, kwenye Tawi moja lililopo Magomeni, zaidi ya kadi 500 za CCM zilirudishwa na wanachama wake na kuchukua za CUF papo hapo kutokana na kutoridhishwa na mchakato mzima wa zoezi hilo.

Tutaendelea kuwaletea updates za matokeo... Endelea kuhabarika