Monday, August 9, 2010

DK. SLAA AKABIDHIWA MIKOBA YA URAIS, ATANGAZA VITA NA CCM



Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbrod Slaa leo amekabidhiwa rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Dk Slaa baada ya kukabidhiwa fomu hizo akiwa na Mgombea Mwenza, Said Mzee Said, amesema kuwa sasa CCM wakae chonjo kwa maana chama chake kimejizatiti kuchukua Madaraka ya nafasi hiyo nyeti kutokana na maandalizi makubwa iliyoyafanya kipindi hiki ukilinaganisha na chaguzi mbalimbali zilizopita.

HONGERA FAHIM! MIEZI MITANO SI MIDOGO!!



Zilikuwa Siku, Wiki na sasa ni Miezi mitano tangu ulipozaliwa,
Mungu akupe uhai, ufike mbali ukubwani, Maisha ni Mitihani,
Hongera Fahim mwanangu, Miezi Mitano umeitimiza!

HAPA NDIPO ANAPOANDALIWA PWEZA?



Mkazi huyu wa jijini Dar es Salaam alikutwa na blogu hii akiandaa samaki aina ya pweza na ngisi kwenye mazingira machafu leo asubuhi, Soko la Samaki Magogoni (Feri). Maandalizi ya chakula kwenye mazingira ya aina hii ni hatari hasa ukuzingatia mtumiaji ni binadamu mimi na wewe.

Mamlaka zinazohusika na masuala ya usafi wa mazingira kwenye maeneo nyeti hasa Sokoni hazina budi kuchukua tahadhari kwa kufanya ziara za mara kwa mara maeneo hayo kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata taratibu na kanuni za usafi wakati wakiandaa bidhaa zao ili kuepusha maradhi ya milipuko kwa watumiaji.

Friday, August 6, 2010

WAZIRI LI DONGDONG WA CHINA ATEMBELEA TSN



Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya TSN inayochapisha magazeti ya Serikali ya Daily News na Habari Leo, Mkumbwa Ally (kushoto) akimtembeza mgeni wake, Naibu Waziri wa Uchapishaji na Habari wa China, Bi. Li Dongdong kuangalia shughuli za uzalishaji wa magazeti hayo ndani ya ofisi za Kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam leo asubuhi. [Picha: kwa hisani ya Yusuf Badi wa TSN]

SHEIN AFUNGUA UJENZI KITUO CHA AFYA BUMBWI SUDI



Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Wananchi wa kijiji cha Bumbwi Sudi kiliopo katika Wilaya ya Magharibi Unguja leo. jumla ya shilingi miloni 25.4 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho. [Picha: Kwa hisani ya Amour Nassor wa VPO]

KITI CHA KWANZA CHA SPIKA WA BUNGE LA TANGANYIKA LA MWAKA 1962


Hiki ndo' kiti cha kwanza cha Spika wa Bunge ambacho kilitolewa kama zawadi na Bunge la  Uingereza (House of Common) kwa Bunge la Tanganyika mwaka 1962 mara baada ya Uhuru. Kiti hiki kimetumika nchini mpaka mwaka 2005. [Picha: kwa hisani ya Owen Mwandumbya wa Bunge].

Monday, August 2, 2010

MTIKILA AYEYA JELA MIEZI 6

Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha DP amedakwa leo na makachero waliokuwa wakimsaka muda mrefu huku wakiwa na 'kibali cha kumkamata' na kufikishwa Mahakama ya wilaya Ilala ambako alikuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita hapo awali.

Mtikila ambaye alionekana kutoamini jambo hilo huku akionekana mwenye kujiamini zaidi, alikuwa akidaiwa deni la zaidi ya shilingi milioni 9 na mkazi mmoja wa jijini hapa Dar es Salaam, Mama Pascazia Zelamula Matete (61) ambaye kitaaluma ni Mwalimu.

Kwa mujibu wa Mama Pascazia, alimkopesha fedha hizo ili ziweze kumsaidia kwenye biashara zake, lakini imekuwa ngumu kwa Mtikila kurudisha fedha hizo kiasi cha kumsababishia mama huyo kutengwa na familia yake hususan mumewe ambaye alimwambia atamrudia tu endapo atakuwa amerudishiwa fedha hizo.


Mtikila akiingia kwenye gari la Polisi kuelekea kituo cha Msimbazi leo

"Hata watoto wangu nao wamenitenga, sasa naishi maisha magumu, nimetengwa na mume wangu, watoto wangu sababu ya huruma yangu ya kumsaidia Mtikila. Leo siondoki hapa, nitafia hapahapa mpaka fedha zangu azirudishe." Alisema mama huyo.

Mtikila alichukuliwa na gari la Polisi wa Kituo cha Msimbazi na kupelekwa kituoni huko kwa ajili ya kuhifadhiwa bada ya muda wa mahakama kuwa umekwisha na anatarajiwa kupelekwa jela kwa kipindi cha miezi sita, jambo ambalo binafsi ameridhia.