Monday, February 7, 2011

CUF WAANDAMANA KUPINGA SERIKALI KUILIPA DOWANS


Wafuasi wa Chama cha wananchi (CUF) wakiandamana kuipinga Serikali kuilipa kampuni ya kuzalisha umeme ya DOWANS shilingi bilioni 94, Dar es Salaam leo asubuhi. PICHA: YUSUF BADI

WANAFUNZI UDSM WAPIGWA MABOMU YA MACHOZI WAKIDAI SH 10,000 YA 'BOOM'

Askari wa kutuliza ghasia 'ffu' leo mchana wamewavurumishia mabomu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuisha kwa mkutano wao na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa uliokuwa ukijadili ongezeko la kiwango cha fedha za kujikimu 'Boom' kwa wanafunzi hao.

Muda mfupi baada ya kuondoka kwa waziri huyo, wanafunzi hao walianza kuwaandama askari hao waliokuwa wakiondoka eneo hilo kwa kuwarushia mawe, chupa za maji na vitu vinginevyo, na kuwazomea jambo ambalo lilizua tafrani kubwa baina ya askari na wanafunzi hao na kulazimika kufyatua mabomu ya machozi kwa mfululizo kwa wanafunzi hao waliokuwa wakivurumisha mawe kwa mfululizo.

Hata hivyo askari hao walifanikiwa kutawanya maelfu ya wanafunzi hao waliokuwa wakiwazonga askari hao waliokuwa na magari maalumu aina ya Defender na Land Cruiser, na kuacha wengine wakiwa wamezimia na wengine kujeruhiwa na mabomu hayo.

Awali katika mkutano wao wanafunzi hao na waziri Kawambwa, walimtaka waziri huyo atoe tamko la ongezeko la kiwango cha fedha hizo kutoka shilingi 5,000 ya sasa mpaka 10,000 waliyokuwa wakidai, jambo ambalo lilimpa wakati mgumu waziri huo kulitolea uamuzi wa moja kwa moja, ambapo kila alipokuwa akizungumzia 'mchakato' wanafunzi hao walikuwa wakizomea na kusema "Hatutaki siasa, tunataka elfu kumi tu."

Hata hivyo Waziri Kawambwa alilazimika kuahirisha mkutano huo baada ya hali kuanza kuwa tete pale wanafunzi hao walipoanza kufanya fujo huku wakimlazimisha atoe tamko litakalowaridhisha wanafunzi hao. "Mimi nimewasikia, nitaenda kushauriana na Hazina tuone namna gani tunaongeza kiwango hcho, lakini si elfu kumi kama mnavyodai.." Alisema hivyo waziri Kawambwa na kusababisha maelfu ya wanafunzi hao waliokuwa wakimsikiliza kuanza kupiga kelele kwa kusema "tunatakaa, aashuukee... Tunataakaa, aashuukee..." na ndipo waziri kawambwa alipoufunga mkutano huo na kuondoka huku akiwaacha wanafunzi hao wakiwa na maswali mengi ya kujiuliza.

Muda mfupi baada ya waziri Kawambwa kuondoka eneo hilo, wanafunzi hao walihamishia hasira zao kwa askari wa kutuliza ghasia 'ffu' kwa kuanza kuwavurumishia mawe, chupa za maji na vitu vingine huku wakiwazomea, jambo lililopelekea askari hao kuanza kufyatua mabomu ya machozi kwa mfululizo na kupelekea eneo hilo kugeuka na kuwa la vita, huku vishindo vikubwa vya mabomu hayo vikisikika na kusababisha moshi mwingi kutanda angani.

HABARI PICHANI:









Wednesday, January 19, 2011

SIKU YANGA ILIPOITOA JASHO ATLETICO PARANAENSE YA BRAZIL


Godfrey Bonny wa Yanga akibadilishana jezi na Bruno Batista baada ya mchezo kuisha


Salum Telela wa Yanga akimtoka Bruno Batista


Rais wa RBP, Rahma Al Kharoosi akizungumza na wanahabari baada ya mchezo


Mabeki wa Atletico wakiwa wameduwaa huku kipa akiwa chini baada ya Bruno Costa De Souza (6) kujifunga


Wachezaji wa Yanga wakibadilishana jezi na wa Atletico ikiwa ni ishara ya 'fair play' baada ya mechi


Kipa wa Atletico, Aderbar Melo dos Santos Neto, akiokoa moja ya hatari langoni kwake huku mabeki wa klabu hiyo wakiwa tayari kwa lolote


Davis Mwape wa Yanga akiwania mpira na beki wa kushoto wa Atletico, Bruno Costa de Souza

Tuesday, November 16, 2010

PINDA NDIYE WAZIRI MKUU


Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amemtangaza Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano iliyobaki.

Spika Makinda alimtaja Mheshimiwa Pinda kuwa Waziri Mkuu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kupitia waraka wake aliomuandikia spika huyo na kusomwa mbele ya wabunge wa bunge hilo leo jioni.

"Nachukua fursa hii kumtangaza Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania." Alisema spika Makinda wakati akisoma barua hiyo iliyotumwa kwake.

Monday, November 15, 2010

WANAJESHI WA UINGEREZA WATOA MAFUNZO YA KUPAMBANA NA MAHARAMIA KWA WANAJESHI WA TANZANIA

Askari wa Jeshi la wanamaji wa Uingereza wamo nchini kwa siku tano ambapo wataendesha mafunzo ya kijeshi kwa askari wa jeshi la wanamaji hapa nchini ya namna ya kupambana na maharamia.

Askari hao waliowasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kwa meli ya kivita ya HMS Montrose watakuwepo kwa siku tano kabla ya kuondoka, ambapo vikosi mbalimbali vya wanamaji wa Tanzania vitapewa mbinu na mafunzo ya namna ya kupambana na maharamia.

Wakiwa njiani kuja hapa nchini, askari hao wameweza kudhibiti maharamia wa somalia kwa kiwango kikubwa. Kamanda wa meli hiyo, Jonathan Lett anasema, "Tumeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa maharamia katika pwani ya Somalia." Alisema.



British Royal Navy soldier, Rob McMurrich with his General Purpose Machine Gun

Sunday, November 7, 2010

MAJERUHI CHENGE ATANGAZA KUGOMBEA USPIKA



Mbunge mteule wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ametangaza azma yake ya kugombea bafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Dar es Salaam.

Chenge ametangaza azma yake hiyo mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini alipofanya nao mkutano kwenye hoteli ya Courtyard, eneo la Upanga Sea view, majira ya saa sita mchana.

"Nimewaita hapa leo ndugu zangu kwa lengo moja tu la kutangaza azma yangu ya kugombea nafasi ya Uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili niweze kutibu majeraha makubwa yaliyoumiza Bunge, Taifa na wananchi wa chama changu (CCM). Mimi kama ilivyo kwa wengine ni miongoni mwa majeruhi wa uongozi, Kama bunge, hatuna budi kukabiliana nalo kwa nguvu kubwa." alisema na kuongeza,

"Bunge letu limekuwa na changamoto kubwa katika miaka mitano iliyopita. Viongozi ambao wajibu wetu ni kuonesha njia badala yake tumekuwa vinara wa uzushi, uongo, fitna na majungu. Mimi ni mwarobaini (dawa ya kutibu) wa majeraha hayo, ambaye naamini ni kiongozi bora na nina uwezo na nia thabiti." Alisema

Sunday, October 31, 2010

BURIANI ELVIS MUSIBA



Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA), Elvis Musiba amefariki dunia leo kwenye hospitali ya TMJ, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ndugu wa familia hiyo, marehemu Musiba alikutwa na mauti hayo majira ya saa nne asubuhi hospitalini hapo kutokana na maradhi ya mguu yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

Marehemu Musiba alikuwa akisumbuliwa na maradhi hayo ambapo mwezi oktoba mwaka huu alipelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kabla ya kufikishwa hospitalini hapo Jumamosi ya wiki iliyopita kwa mujibu wa ndugu hao.

Taratibu za mazishi zinafanywa nyumbani kwa marehemu Mikocheni, Dar es Salaam.

Marehemu Musiba katika uhai wake aliwahi kuwa Mtunzi mashuhuri wa simulizi za riwaya ambazo ni pamoja na 'Kufa na Kupona, Kikomo, Kikosi cha Kisasi, Njama na Hujuma na nyinginezo ambapo pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali za wakurugenzi zikiwemo Sematel Ltd (DRC), Exclusive Lodges Resort Ltd, Kamati ya Mahesabu ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Akaunti ya Milenia (Tanzania) na Kituo cha Uwekezaji cha TIC.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali pema Peponi, Amina.