Thursday, April 21, 2011

OPERESHENI YA SHIRIKA LA NYUMBA YAMKUMBA OFISA MSTAAFU WA USALAMA WA TAIFA


Leo majira ya saa nne asubuhi, kwenye mtaa wa Uhuru, nyumba namba 102 ya Shirika la nyumba (NHC), ilikuwa ni siku mbaya kwa familia ya Ofisa Mstaafu wa Usalama wa Taifa, aliyefahamika kwa jina la Aboubakar Kapera baada ya vibarua wa kampuni ya udalali ya Kimbembe kuvamia makazi yake na kuanza kuhamisha vyombo nje kwa ajili ya kuvipiga mnada.

Operesheni hiyo iliyo chini ya NHC, ni ya kukusanya madeni yake kwa wadaiwa sugu ambao wameshindwa kulipa kodi zao kwa muda mrefu.

MPIGANIA UKOMBOZI WA KOSOVO AONDOKA NCHINI KUELEKEA BURUNDI KUENDELEZA KAMPENI YAKE

Kapteni James Bareshi, ambaye ni raia wa jimbo la Kosovo lililo chini ya utawala wa Urusi ameondoka leo nchini kuelekea Burundi kuendeleza harakati zake za kampeni ya kutaka jimbo hilo kuwa nchi inayojitawala yenyewe.

James, ambaye anatumia ndege ndogo ya abiria watatu yenye ujumbe unaosomeka "PLEASE RECOGNIZE THE INDEPENDENCE OF KOSOVO" anatembelea nchi mbalimbali duniani kusambaza ujumbe wake huo. Juzi James, alikuwa hapa nchini ambapo alikutana na vyombo mbalimbali vya habari akizungumzia azma yake hiyo ya kutaka Kosovo kuwa nchi huru.



Kwa mujibu wa msaidizi wake ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema kuwa, James hutua ardhini kila baada ya saa nne kwa ajili ya kuongeza mafuta kwenye ndege yake ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na safari inazokwenda.

James, ambaye ni 'PILOT' kitaaluma, anapata ufadhili wa raia wa Kosovo wanaoishi maeneo mbalimbali ya dunia kwa kufanya harambee kwa ajili ya kuhakikisha anafanikisha zoezi lake hilo.



Ndege ndogo anayotumia James Bareshi kusafiria

TTCL WATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA MILIPUKO GONGO LA MBOTO

Kampuni ya simu ya TTCL leo imekabidhi msaada wa vyakula mbalimbali kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Leonidas Gama kwa niaba ya waathirika wa milipuko ya mabomu, Gongo la Mboto leo.

Lakini kwa mtazamo wangu, hawa wanaotoa misaada kwa waathirika wa milipuko ya mabomu Gongo la Mboto ni vema sasa wakabadilisha aina ya misaada na badala yake wakaenda kuona ni kwa kiasi gani wanavyoathiriwa na mvua za Masika zinazoendelea kunyesha hapa jijini.

Naamini, wengi wao bado wanaendelea kulala kwenye mahema, ambayo kwa kiasi kikubwa hayawezi kuhimili mikiki mikiki ya mvua hizi kwa sasa. Wengi wa waathirika hao, ni wale wenye familia wakiwemo watoto wadogo ambao naamini kwa kiasi kikubwa ndiyo waathirika wa mvua hizi.

Hivyo licha ya wahisani kuendelea kuonyesha moyo wa upendo kwa kutoa misaada, ni vema sasa wakaangalia upande wa pili hasa msimu huu wa mvua za masika.



Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Leonidas Gama akikabidhiwa msaada wa vyakula na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu nchini TTCL, Said Amir Said

DK SHEIN AKUTANA NA BALOZI DIANNE CORNER WA UINGEREZA IKULU ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianne Corner, Ikulu Zanzibar leo

Pics/source: Ikulu, Zanzibar

SALMA KIKWETE ATEMBELEA THUNDERBIRD SCHOOL OF GLOBAL MANAGEMENT, ARIZONA, MAREKANI

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Salma Kikwete yupo nchini Marekani akiendelea na ziara yake kwenye majimbo mbalimbali ya nchi hiyo. Leo Mama Salma alitembelea shule ya Thunderbird pamoja na kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo.


Salma Kikwete akizungumza na kujibu maswali mbalimbali ya wanafunzi wa shule hiyo (hawapo pichani)


Salma Kikwete akiongozwa na Mwenyeji wake, ambaye ni Rais wa shule hiyo, Dk Angel Cabrera kuangalia eneo la shule hiyo

Pics/Source: Mwanakombo Jumaa, Maelezo

Monday, April 18, 2011

ZA MWIZI AROBAINI



Wakazi wa Buza Cape Town, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam wakiangalia mwili wa kijana mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Iddi ambaye ni mkazi wa Buza Kinyantira aliyeuawa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za wizi.

Kijana huyo anadaiwa kufumwa akiiba kuku katika moja ya banda la kuku huko Buza, ambapo wananchi hao walianza kukumponda kwa mawe na vitu vizito mpaka kupelekea kifo chake.

Hata hivyo baadaye, askari polisi waliuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi kwenye chumba cha Maiti cha hospitali ya Temeke jijini, ambapo ndugu zake walikuja kuuchukua kwa mazishi.

PIC/SOURCE: Inno

MARAIS AFRIKA MASHARIKI WAKUTANA KUJADILI UCHUMI WA AFRIKA

Marais watano wa nchi za Afrika Mashariki leo wamekutana kwa mara ya tisa kujadili maendeleo ya ukuaji wa uchumi kwa nchi zao, kwenye ukumbi wa mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam leo.

Mkutano huo wa tisa wa uwekezaji barani Afrika umewakutanisha marais, Jakaya Kikwete wa Tanzania, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Mwai Kibaki wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Dk Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Rwanda, Bernard Mukuza.



Marais hao wakiwa kwenye mkutano huo