Sunday, August 30, 2009

MWEZI WA RAMADHAN: Bei za Vyakula wala hazijapanda kiviiile..

Si ajabu kukuta watu wakilalamikia kuhusu kupanda kwa bei za vyakula kila unapofika mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ukiuliza wafanyabiashara kwa nini bei za vyakula hasa vile vya futari kama ndizi, mihogo, viazi, maharage na vinginevyo vinapanda bei, watakwambia gharama za usafirishaji zipo juu.

Wengine watakwambia wakulima wenyewe ndio wanaopandisha bei za mazao huko mashambani. Lakini kwa ujumla ukiangalia harakaharaka utagundua kuwa imekuwa ni kama 'fasheni' kwao kufanya hivyo kwa misingi ya ki'maslahi' yao binafsi.

Wanajua kuwa hata ufanyeje lazima tu utanunua mihogo ama ndizi kwa ajili ya kwenda kutengeneza futari, hivyo huna njia ya kukwepa... Lakini hili linawezekana kukemewa na kusimamiwa ipasavyo na Mamlaka za masoko na hali ikawa shwari kabisa.

Ukiliangalia suala hili kwa misingi ya kimatabaka, utagundua kuwa tabaka la watu fulani ndilo linaloathirika zaidi na upandishwaji wa bei za vyakula hivi, wakati tabaka fulani haliathiriki kutokana na tofauti ya vipato.

Tuachane na hilo, lakini jana nilitembelea katika masoko mawili maarufu kwa vyakula hivi, soko la Temeke Stereo na la Buguruni, hali nilikuta tofauti. Kwa kweli bei za vyakula hazikuwa za kutisha zilikuwa ni za kawaida tu, mfano fungu moja la mihogo lilikuwa ni kati ya sh 500 na 1000, wakati ndizi moja ya mzuzu iliuzwa kati ya 200 na 250 bei ambazo ni za siku zote.

Niliwauliza wafanyabiashara kuwa kwa nini wakati watu wanalalamika huko mitaani kuwa bei za vyakula zipo juu , hali ni tofauti katika masoko hayo walinijibu kuwa, tatizo hawatembelei masokoni na badala yake wanatembelea kwenye magenge na ndo maana wanalalamika kuwa bei za vyakula zimepanda.

Nikagundua kuwa, alaa kumbe watu hawana utamaduni wa kutembelea masoko kama haya na kuishia kulalamikia kupanda kwa bei za vyakula... jamani tutembeleeni masoko yetu ili tukanunue bidhaa zetu kwa bei nafuu..



Wafanyabiashara za ndizi wakiwajibika sokoni Buguruni


Wananchi wakinunua mihogo sokoni Buguruni

ARE WE SAFE?

Hii ni chemchem ya maji machafu inayotiririkia katika bahari ya Hindi, eneo la Ufukwe wa Gymkhana, Dar es Salaam. Eneo hili lina umuhimu sana kwa watoto na hata wakubwa kwa kuja kujipumzisha siku za mwisho wa wiki.

Wakati mwingine watoto hawa na wakubwa huogelea kwa ajili ya kupunguza joto la jiji hapa. Lakini hatari iliyopo na ambayo huenda tayari imeshajitokeza kwa watoto hawa na wakubwa, ni magonjwa ya kuambukizwa, mfano ngozi, homa za matumbo na kadhalika.

Hii inatokana na kiasi kikubwa cha maji wanayotumia kwa kuoga kuathiriwa na majitaka kama si ya 'kinyesi' yanayotirikia katika ufukwe huo. Haiyumkini maji haya yanatoka wapi, lakini harufu yake kali inatosha ku'define' kuwa maji haya si salama hata kwa kuvuta harufu yake.

Sihitaji kuuliza kama Mamlaka husika imeliona hili ama la, lakini wajibu wangu kama mpashaji wa habari na matukio nachukua fursa hii kuzihoji Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini hapa (DAWASA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji, (Dar es Salaam City Council) kama wanalifahamu hili ama la, na kama wanalifahamu kuna hatua gani zinachukuliwa kunusuru hali hii?


"Haya ndiyo majitaka yanayoingia baharini..." ni kama anaonesha ishara ya kusema hivi huyu mkazi...

BOMU JINGINE LALIPUKA MBAGALA

WAKATI waathirika wa mabomu yaliyotokea eneo la Mbagala Kuu karibu na kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiendelea kulipwa fidia zao juzi kulitokea mlipuko na kusababisha baadhi ya wakazi hao kukimbia.

Mlipuko huo ulitokea juzi saa 1:30 usiku mtaa wa Mbagala Kuu baada ya msimamizi wa nyumba hiyo Elisi Emmanuel kukusanya uchafu na kuchoma takataka kwenye nyumba yenye namba MA/1/2835 na kujiandaa na ujenzi upya.

Emmanuel ambaye hakumtaja mmiliki wa nyumba hiyo alisema alikuwa anafanya usafi saa 11:00 jioni na baada ya kufanya usafi huo aliondoka kwa muda lakini ulipofika saa ilipofika saa 1:30 usiku ghafla kulisikika mlio mkubwa hali iliyopelekea waathirika ambao walikuwa mamemaliza kufturu kutokana na mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan kukimbia ili kujinusuru na maisha yao.

**Veronica Mheta**

AMA KWELI KUFA KUFAANA...


Watoto, wakazi wa mbagala eneo la msikitini wakichota maji katika bomba lililopasuka kama walivyonaswa na kamera yetu leo mchana.

Wednesday, August 26, 2009

KUTOKUSOMA VITABU KUNACHANGIA UMASIKINI

Wananchi wametakiwa kusoma vitabu zaidi ili kujikwamua na umasikini.

Mtunzi wa kitabu cha 'The Bleeding Heart and Other Poems', Shilia Kaaya ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kitabu chake hicho, leo Dar es Salaam.

"Ukitaka kumficha jambo mwafrika, liweke kitabuni. Kama unasafiri safari ya mwendo mrefu, jitahidi usome angalau kitabu kimoja, mpaka unafika safari yako utakuwa mtu mwingine tofauti." Alisema Kaaya.

Kitabu cha 'The Bleeding Heart and Other Poems' kitaanza kusomwa na wanafunzi wa kidato cha tano na sita kote nchini baada ya kupitishwa na kamati ya wataalamu ya Wizara ya Elimu.


Mtunzi wa kitabu cha the bleeding heart... Bw. Kaaya


Kitabu cha the bleeding heart

Friday, August 21, 2009

WAPYA 214 WAJIUNGA CCM

JUMLA ya wanachama wapya 214 wamejiunga na chama cha ccm leo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa bakhressa, manzese, jijihi hapa.

Wanachama hao wengi wao wametokea katika chama cha TLP, CUF na CHADEMA.

Wakizungumnza kwa nyakati tofauti mara baada ya kukabidhiwa kadi mpya za CCM, wanachama hao wamesema kuwa sababu ya kujiunmga na CCM ni kutokana na demokrasia iliyopo ndani ya chama hicho ambayo wamesema ni ya kweli ukilinganisha na vyama walivyokuwa awali.


sehemu ya wanachama 214 wapya wa CCM wakila kiapo baada ya kujiunga na chama hicho leo


'Ukitaka kujua utamu wa ngoma, ingia ucheze...

Thursday, August 13, 2009

mbio za Ligi Kuu- Vodacom wamwaga vifaa vya michezo vilabuni...

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa ligi kuu ya vodacom tanzania bara, Kampuni ya simu za mkononi Vodacomleo imemwaga vifaa vya michezo vya mabilioni ya shilingi kwa vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo.


Lucas Kisasa ambaye ni katibu wa Yanga S.C akipokea vifaa vya michezo toka kwa naibu waziri wa habari, utamaduni na michezo, joel bendera leo katika hoteli ya giraffe jijini hapa...


Katibu wa Simba Mwina KAduguda naye akipokea vifaa hiyvo...


Hassan Mazala mwenyekiti wa African Lyon pamoja na Katibu wake, Jeshi Zakaria nao wakipokea vifaa hivyo toka kwa naibu waiziri wa habari, utamaduni na michezo, mh. joel bendera...

Hepi besdei tu yuuu....




Wafanyakazi wenzangu, Albina, Kingoba na Jane wakinilisha keki ya hepi besdei yao ya kutushtukiza leo ofisini... hata hatukujua wametimiza umri gani...

Friday, August 7, 2009

JIJI, USALAMA WA AFYA ZETU UNAZINGATIWA?

Hali ya usafi katika soko la samaki Magogoni (Ferry) si ya kuridhisha. Hii imekuwa ni hali sugu sasa kutokana na kutofanyiwa kazi kama si kumalizwa kabisa kwa tatizo hili, sokoni hapo.

Si jambo la kustaajabisha kushuhudia mitaro ya maji machafu yenye harufu kali ikitiririkia baharini wakati mvuvi akiwaosha samaki wake katika maji hayo kabla ya kupeleka kwa wanunuzi..

Lakini hili lisionekane kama ni tatizo la kawaida kwa maana mimi na wewe ambao tunakifurahia kitoweo cha samaki wa baharini hasa wale wanaotoka sokoni hapo hatujui mpaka sasa usalama wa afya zetu ukoje?

Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na Mamlaka husika inayosimamia shughuli za uendeshaji wa soko hilo hauna budi kuliangalia hili kwa macho mawili, vinginevyo afya zetu haziko salama hata kidogo...



Mchuuzi akipita kwa shida katika mitiririko ya maji machafu yenye harufu kali, inayoingia baharini eneo la uvuvi...


Hali si nzuri.. Angalia mchuuzi huyu wa samaki akipita katika michuruziko hii ya maji machafu yenye harufu kali inayoingia baharini, eneo la soko la samaki...

UNICEF YAIPA SHAVU TANZANIA

Tanzania imetajwa kuwa ni nchi pekee barani Afrika inayosimamia na kulinda haki za watoto wenye mahitaji mbalimbali.

Mjumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)Ghana, Dk Agnes Aidoo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, mchana.

Amesema hiyo imetokana na kuundwa kwa Sheria Mpya ya Watoto inayosisitiza kuwalinda dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili ambayo inatarajiwa kujadiliwa na wadau mbalimbali ili iweze kupitishwa Bungeni mapema mwaka huu.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati za kutetea Haki ya Mtoto (CRC) toka nchini Ghana, Dk. Agnes Aisoo


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margaret Sitta

Thursday, August 6, 2009

Mkenya mwanamama anaswa Ubungo stendi na dawa za kulevya..

Amini usiamini... Mama mmoja raia wa Kenya, aliyefahamika Kwa jina la REBECCA WAIRIMU amenaswa na UNGA wa dawa za kulevya aina ya HEROIN pale Ubungo Bus Terminal, jana jioni na mashushu wa kibongo...

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya, ACP Godfrey Nzowa, mama huyo alikuwa akitokea Kenya kwenda SOUTH AFRICA kwa mzee ZUMA huko kwa ajili ya kutafuta soko la dawa hizo..

Mara baada ya kushuka stendi ya ubungo jana jioni, mashushu wakamtilia mashaka na kuanza kumpekua... ndipo walipomkuta na dawa hizo. unga huo unakadiriwa kuwa na uzito wa kilo 3 na thamani yake bado haijajulikana...

Kwa sasa mama huyo anashikiliwa na mashushu hao... na mara baada ya uchunguzi kukamilika kama atabainika na makosa basi atafunguliwa mashtaka...


Na hivi ndivyo mama huyo alivyoficha hayo madawa ya kulevya aina ya Heroin... Hapa Mkuu wa kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya nchini, ACP Godfrey Nzowa akizitafuta dawa hizo baada ya kubaini... Anaanza kwa kutoa nguo zilizomo ndani ya begi..


kisha nguo zote zimekwisha.. sasa 'unga' uko wapi?... hebu angalia sasa picha ya chini uone namna mwanamama huyo alivyokuwa ameuficha UNGA huo kwa chini kwabisa ili usigundulike...


Amini usiamini... huu ni mfuko ambao umenakshiwa kwa kahawa na ndani yake sasa ndio kuna unga wa dawa za kulevya aina ya HEROIN...


Hii ni pasipoti yake ya kusafiria...

Mambo ya Kibajaj haya hapa...

Duh... ukimuangalia jamaa kama anaendesha ki'bajaj' vile eeh! sasa kumbe, unataka kubisha. Hawa jamaa niliwakuta pale mtaa samora katikati ya jiji wakiburudisha wananchi. Lakini sio burebure tu... unadondosha 'kwenzi' au 'noti' kwenye kisahani burudani inaendelea... hebu wacheki hapa chini...


nanyonga kibajaj... nanyonga kibajaj eeh...

Mlalahoi anyakuwa Mil.5 za Kismat sms

Waswahili wanasema ukilala masikini utaamka tajiri... ndivyo ilivyo kwa mama huyu Baby Sheni mkazi wa Igunga, Tabora amejinyakulia sh milioni 5 za halali katika mchezo wa bahati nasibu ya Kismat sms wakati wa droo ya pili ya mchezo huo leo hapa uliochezwa katika ofisi za Selcom gaming jijini hapa... na hiyo chini ni picha ya mchezo huo...

Meneja masoko wa Selcom gaming, Juma Mgori pamoja na Humudi Abdulhusein wa Bodi ya michezo ya kubahatisha wakiongea na mshindi..