Thursday, April 16, 2009

Kwa heri Kandoro, karibu Lukuvi na hizi ndizo changamoto zetu..

Aliyekuwa Mkuu wa mkoa huu wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro amehamishiwa mkoani Mwanza kikazi ambapo mikoba yake sasa imechukuliwa na William Lukuvi aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma. Hapana shaka Kandoro atakumbukwa kwa mengi mema yake aliyoyafanya katika jiji hili lenye changamoto lukuki, akiwa na dhamira ya kujaribu kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.

Changamoto ambazo bado zinaukabili mji huu ni nyingi. Lakini zipo zile changamoto kubwa kubwa ambazo ni tatizo la maji, umeme, usafiri, msongamano wa majumba na watu na kadhalika.

Ninavyofahamu mimi, hata angeletwa binadamu wa aina gani kuongoza miji mikubwa kama huu wa Dar es Salaam, bado atakuwa anakabiliwa na changamoto mbalimbali na si kutatua zote kama wengi wetu tunavyodhani. Ni dhahiri shahiri, watanzania tulio wengi tunatamani kuwa na maisha mazuri kwa muda mfupi sana, hilo halina ubishi.

Hivyo inatupasa kumshukuru Kandoro kwa aliyoyatenda katika kipindi cha uongozi wake jijini hapa. Wapo wenzangu watakaomtoa kasoro kulingana na utashi wao, wapo watakaokuwa hawana maoni yoyote wale wenzangu wa 'no comments', na pia wapo ambao wapowapo tu, hata ukiwauliza utamkumbuka Kandoro kwa lipi alilolifanya hapa jijini, wao watakwambia 'kwa mengi tu' halafu ukiwaambia wakutajie hata moja, watakujibu 'sikumbuki'.

Mji huu ni mkubwa, ukilinganisha na mingine. Ninapozungumzia ukubwa namaanisha mzunguko wa hela katika mji huu ni mkubwa sana kutokana na kuwepo kwa vyanzo vingi vya mapato ya Serikali ukilinganisha na miji mingine. Bandari, Reli, Barabara, Uwanja wa ndege, Viwanda, Maduka makubwa, na vinginevyo ni miongoni mwa vyanzo hivi vya mapato ya Serikali yanayofanya mzunguko mkubwa wa hela.

Hivyo basi, kutokana na hayo yote, wananchi wengi hukimbilia mji huu kujitafutia ajira na wengine kujiajiri wenyewe. Mbali na hilo, pia wawekezaji wengi wamekimbilia mji huu kuwekeza kutokana na kuwepo kwa angalau mazingira mazuri ya uwekezaji. Hivyo ni dhahiri kuwa, changamoto katika mji huu si jambo la kulishangaa, bali pia ni sehemu ya maisha katika mji huu.

Hili linanifanya sio tu kumnyooshea kidole Mheshimiwa Kandoro eti 'mbona jambo fulani halijatekelezwa' bali pia kuamini binadamu sisi kamwe hatuwezi kulingana na malaika wa mbinguni. Hivyo, kuhamishwa ghafla kwa Mheshimiwa Kandoro toka jijini hapa na kwenda Mwanza, kunadhihirisha wazi kuwa hakuwa mtu wa kubabaisha tu kutokana na mabadiliko aliyoyafanya katika mji huu ukilinganisha na awali. Kila kiongozi aliyepita alifanya mabadiliko yake kwa wakati wake.

Hivyo amehamishiwa jijini Mwanza pia, kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika taswira ya jiji pamoja na wakazi wake kwa ujumla. Tunakutakia kila la kheri huko uendako mzee wetu Abbas Kandoro, na karibu jijini Dar es Salaam Mheshimiwa William Lukuvi, na hizi ndizo changamoto zetu..


Abbas Kandoro, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment