Tuesday, May 12, 2009

HATUNA MPANGO WA KUJENGA KAMBI YA KIVITA YA KIJESHI TANZANIA- MAREKANI

Kamanda wa kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Marekani kwa Afrika, General. illiam Ward amekanusha taarifa kuhusu mpango wa nchi hiyo kujenga kambi ya kivita ya jeshi la hnchi hiyo hapa Tanzania.

General Ward amesema misaada inayotolewa na Marekani kwa Jeshi la Ulinzi la Tanzania haina maana ya kushawishi jeshi hilo kujenga kambi ya kivita ya nchi hiyo hapa nchini, kama baadhi ya taarifa zinavyodai.

General Ward alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari wa Tanzania katika chumba cha mikutano cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ- Makao Makuu), Upanga Dar es Salaaam leo, wakati wa hafla ya kukabidhi magari maalumu ya 'Deraya' yatakayobebea wapiganaji wa kijeshi watakaokwenda Darfur, nchini Sudan hivi karibuni kulinda amani.

"Hizo ni taarifa za kizushi tu." Alisema.

General Ward alisema Marekani na nchi wanachama inafanya juhudi mablimbali za kulinda amani katika nchi za Afrika zilizo katika mizozo ya kivita, na si lengo kujenga kambi za kivita za kijeshi kama inavyodhaniwa na wengi.

Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Uingereza leo walikabidhi magari maalumu yanayojulikana kwa jina la 'Deraya' pamoja na vitu mbalimbali vya kijeshi kwa JWTZ, yatakayosaidia kikosi maalumu kitakachokwenda Darfur, Sudan kulinda amani hivi karibuni.

Jumla ya askari 875 wa JWTZ, wanatarajiwa kwenda Darfur, nchini Sudan kwa ajili ya kusaidia kulinda amani ikiwa ni mkataba wa makubaliano uliotiwa saini na Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa, jijini hapa leo.

Katika askari hao, 800 wataingia moja kwa moja katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kusimamia ulinzi na amani katika vituo viwili vya KO-Abeche pamoja na Mujahiriya vyote vya jimbo la Darfur, wakati askari 75 ni wahandisi wa Jeshi ambao watakuwa wakisimamia shughuli zote za ujenzi wa Jeshi hilo litakapokuwa nchini Sudan.

Wakati huohuo, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Lt. General Abdullrahman Shimbo amevitaka vyombo vya habari nchini kutopotosha taarifa zozote zinazohusiana na mambo ya kijeshi kwa wananchi kwa ajili ya kutowapa hofu wananchi hao.

Akizungumzia kuhusu tukio la jana jioni la mlipuko wa bomu, Shimbo alisema bomu hilo lililipuliwa na wanajeshi wa kambi hiyo wakati walipokuwa wakifanya usafi wa eneo la kambi na kukuta bomu dogo la kurusha kwa mkono, hivyo hawakuona sababu ya kuwatia hofu wananchi na kuamua kulilipua, jambo ambalo lilikaririwa tofauti na baadhi ya vyombo vya habari.

"Lile bomu halikulipuka lenyewe. Wanajeshi walililipua baada ya kulibaini wakati wakifanya usafi." ALisema.


Magari ya kijeshi ya 'Deraya' yaliyokabidhiwa kwa JWTZ leo

No comments:

Post a Comment