Wednesday, August 25, 2010

JK, DK BILAL WACHANJA MBUGA KWA KASI

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete pamoja na Mgombea Mwenza, Dk. Gharib Bilal wanazidi kuchanja mbuga kwenye kampeni zao za kuomba kura.

Rais Kikwete yeye leo alikuwa Bukoba mjini mkoa wa Kagera akiomba kura wakati Dk. Bilal yeye yupo mkoani Lindi akisaka kura hizo.


Pichani: Rais Jakaya Kikwete akiwa Bukoba mjini leo


Pichani: Dk Gharib Bilal akisalimiana na wakazi wa kijiji cha Mkwajuni, Lindi Vijijini.


Pichani: Wakazi wa Kijiji cha Kilangala wakisikiliza jambo

MADEREVA WAZEMBE SASA KUDHIBITIWA NA TEKNOHAMA



Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema akionyesha mfano wa leseni mpya zilizo kwenye mfumo wa Teknohama zinazotarajiwa kutumiwa na madereva nchini, wakati akifungua semina ya siku mbili kwa Makamanda wa Mikoa na Makamanda wa vikosi vya usalama barabarani na watendaji wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuhusu mchakato wa namna ya utoaji wa leseni hizo mpya, Dar es Salaam leo. PICHA: Hassan Mndeme wa Jeshi la Polisi.

MABADILIKO YA TABIANCHI YAZIDI KULETA ATHARI DUNIANI

Wanaharakati wa masuala ya Mazingira duniani wanaendelea na kampeni yao ya utunzaji wa mazingira ili kuiepusha sayari hii tunayoishi kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.



Lakini hilo linatatizwa na kuongezeka kwa shughuli za kila siku za binadamu zinazochangia kuongezeka kwa athari hizi uniani. Shughuli hizi kama viwanda, ukataji miti na uchomaji misitu na nyinginezo ni sehemu tu ya zinazochangia kupoteza taswira sura ya dunia.

Monday, August 23, 2010

JK MBELE KWA MBELE MWANZA

Rais Jakaya Kikwete ameendelea kukusanya pointi muhimu kwa wananchi zitakazomwezesha kuchaguliwa tena kushika wadhifa huo kwa kuendelea na mikutano yake ya kampeni katika wilaya za Serengeti na Sengerema, baada ya kumaliza Mwanza mjini, mkoani humo.



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia wananchi katika kata ya Nyehunge jimbo la Buchosa, wilaya ya Sengerema  leo mchana.

Sunday, August 22, 2010

NA HII NDIYO ATHARI YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI, KIJANA ACHOMWA MOTO MPAKA KUFA KAMA MNYAMA VILE!

Kijana huyu anayesemekana kuwa mkazi wa Goba ambaye jina lake halikufahamika mara moja alikutwa akiteketea kwa moto eneo la Kimara Mwisho, Dar es Salaam jana baada ya watu wasio na huruma kumchoma moto wakimtuhumu kwa wizi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hili, kijana huyu alishambuliwa na vijana waendesha pikipiki maarufu Bodaboda baada ya kumtuhumu kuiba pikipiki la mmoja wa vijana hao ambapo walimkamata na kuanza kumshambulia kabla ya kumchoma moto hadi kufa kikatili.



Inadaiwa kuwa, kijana huyu ilikuja kufahamika baadaye kuwa hakuwa mwizi kama ilivyodhaniwa na waendesha pikipiki hao bali alifika hapo kwa mafundi akiwa na pikipiki yake kwa ajili ya kutengenezewa na ndipo alipoazima moja ya pikipiki zilizokuwa kwa fundi huyo kwa ajili ya kwenda kuchukulia mafuta kuja kuweka kwenye pikipiki yake.

"Alipokuwa akipita njiani mwenye pikipiki lake akamwona na kuwaambiza wenzake na kuanza kumfukuzia akidhani kaibiwa pikipiki lake hilo," Anasema shuhuda na kuendelea, "Alipofika Kimara Kona aliegesha na kwenda kituoni kuchukua mafuta. Wale jamaa walipofika eneo hilo hawakumuona na kuamua kurudi, lakini wakiwa njiani walimwona tena kijana yule akirudi na pikipiki hilo akiwa amebeba mafuta na ndipo walipomdhibiti na kisha kuanza kumshambulia, kiasha wakamwagia mafuta yake aliyokuwa amebeba na kumuwasha moto." Alisema

Katika hali ya kushangaza, wakati kijana yule akishambuliwa polisi walifika eneo hilo na kisha kuodnoka pasipo kuchukua hatua zozote. Ndipo baadaye polisi wa Mbezi wakiwa na Defender walipowasili hapo kijana wa watu akiwa tayari amekwisha teketea kwa moto.

Ndugu zake kijana huyo walipopata taarifa walifika eneo la tukio na kuthibitisha mwili wa ndugu yao, ambapo walisema kuwa kijana wao hakuwahi kuwa mwizi na yeye alikuwa akijishughulisha na shughuli zake maeneo ya huko Goba.



Hili ni tukio la kusikitisha. Vyombo mbalimbali vimekwishazuia watu kujichukulia sheria mkononi vikiwa na maana nzuri tu kwa jamii. Kama mtu anatiliwa shaka, vyombo vinavyohusika vipo na taarifa zitolewe huko wao watashughulikia. Wahenga wanasema kuwa 'majuto ni mjukuu.' Na hivi ndivyo waliohusika na kitendo cha kumchoma moto kijana huyu wanavyojutia nafsi zao kwa namna moja ama ingine.

Wananchi wenzangu, tuache kujichukulia sheria mkononi. Na hii ndiyo athari kubwa ya kufanya hivyo. Kwa yeyote aliyehusika kwa namna moja ama nyingine aidha kwa kumtupia jiwe kijana huyu au kwa kushabikia wakati kijana huyu akishambuliwa, ajue kabisa nafsi yake inamsuta na kwa Mungu atajibu dhambi zake hizi.

Lakini pia askari polisi ambao hawana weledi na taaluma ya kazi hiyo, hawatufai kwenye jamii. Kwa nini askari waliofika eneo la tukio wakati kijana huyu akishambuliwa wasichukue hatua za kudhibiti hali hiyo, badala yake kulipuuzia na kisha kuondoka zao, huku nyuma wakiacha kijana huyu akichomwa moto kama panya aliyefumaniwa akidokoa kipande cha nyama kwenye chungu.

Na hii ndiyo athari kubwa ya kujichukulia sheria mkononi!!

Monday, August 16, 2010

VODACOM ILIPOFUTURISHA KARIMJEE


Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Dietlof Mare (kulia) akikabidhi ndoo ya mafuta kwa waumini wa kiislam


Akinamama wa kiislam wakifuturu sambamba na Mkurugenzi wa Mahusiano na Vodacom Fouandation, Mwamvita Makamba


Walimu na wanafunzi wa madrasa wakiimba qasida kabla ya kufuturu


Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Dietlof Mare (katikati) akifuturu na waumini wa kiislam


Waumini wa kiislam wakisubiri kufuturu

Hafla hiyo ilifanyika jana jioni kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Issa bin Shaaban Simba na Shehe Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.

Friday, August 13, 2010

CHATU WA KEKO APATIKANA



Chatu aina ya Sebei au 'African Rock Python' mwenye uzito wa kilogramu 8, urefu wa futi 7 na umri wa miaka 6, aliyekuwa amepotea siku kumi zilizopita Wizara ya Maliasili na Utalii, amepatikana leo.

Chatu huyo ambaye alizua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wanaoishi kata ya Keko, jirani na wizarani hapo, alipatikana majira ya saa 6.30 mchana wa leo akiwa amejificha kwenye mazulia mabovu na majenereta, ndani ya eneo hilo la wizara.

Kwa mujibu wa watumishi wa wizarani hapo, chatu huyo alikuwa akikamata panya na kula kwa siku hizo kumi. Lakini pia wamesema hakuna madhara yoyote yaliyotokea.

CHATU PICHANI:



MIGIRO AMUHANI MAREHEMU MZEE KAWAWA



Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro (wa nne kulia) Pamoja na familia ya marehemu Rashid Mfaume Kawawa wakiomba dua katika kaburi baada ya kwenda kutoa pole kwa familia hiyo Madale, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Mke wa Marehemu, Asina Kawawa, Dada wa Marehemu Bi Amina, mtoto wa marehemu Vita Kawawa (wa pili kulia) na Shekhe Abubakar Alli (kulia ambaye ni Imam wa Msikiti wa Kawawa. Picha: Yusuf Badi

FUTARI YA MFUNGO WA RAMADHAN..



Waumini wa kiislamu wa Msikiti wa Al- Islaamiya, Mabibo, Dar es Salaam wakifuturu kama walivyokutwa jana kwenye msikiti huo. Waumini wa dini hiyo nchini na duniani wapo kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao ni moja kati ya nguzo tano za dini hiyo. Picha: Sponsor

MBIO ZA MWENGE TURIANI, MOROGORO



Mfanyabiashara wa mjini Turiani, Wilayani Mvomero, George Kiluwa (katikati) akipokea kiasi cha sh milioni 15 alizokopeshwa na Chama cha Akiba na Mikipo Tursaccos cha Turiani, kutoka kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Dk Nassoro Ally Matuzya (kulia) katika halfa ya kupitiwa na Mwenge wa Uhuru, mwishoni mwa wiki mjini humo. Picha: John Nditi

JK AFUNGUA KIKAO CHA NEC (CCM) LEO



Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, akifungua rasmi kikao cha kamati kuu ya CCM Taifa kilichokutana jana katika ukumbi wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Makao Makuu mjini Dodoma. Picha: Amour Nassor, Ikulu Zanzibar

MAZIWA HAYA NI HATARI KWA WATOTO!



Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo,(kushoto) akionesha kopo la maziwa aina ya NAN 2 kwa waandishi (hawapo pichani) ambayo ni bandia hayafai kwa matumizi ya watoto. Kulia ni Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula Raymond Wigenge. Picha: Yusuf Badi

Tuesday, August 10, 2010

RAMADHAN KAREEM KWA WAISLAM WOTE NCHINI...



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al Hajj Dk Amani Abeid Karume akitoa salamu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa wananchi na waumini wa Dini ya Kiislamu na kuwatakia mafanikio katika ibada hiyo. Picha: Ramadhan Othman wa Ikulu, Zanzibar

JK AZINDUA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA (DART) LEO



Rais Jakaya Kikwete (katikati) akipatiwa maelezo kuhusu ramani ya Miundombinu ya mfumo wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) na Mtendaji Mkuu wa Wakala hao Cosmas Takule (kulia) alipozindua Ujenzi wa Miundombinu hiyo, jana eneo la Kivukoni Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani (kushoto) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, John McIntire

Photo Source: Sponsor

Monday, August 9, 2010

DK. SLAA AKABIDHIWA MIKOBA YA URAIS, ATANGAZA VITA NA CCM



Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbrod Slaa leo amekabidhiwa rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Dk Slaa baada ya kukabidhiwa fomu hizo akiwa na Mgombea Mwenza, Said Mzee Said, amesema kuwa sasa CCM wakae chonjo kwa maana chama chake kimejizatiti kuchukua Madaraka ya nafasi hiyo nyeti kutokana na maandalizi makubwa iliyoyafanya kipindi hiki ukilinaganisha na chaguzi mbalimbali zilizopita.

HONGERA FAHIM! MIEZI MITANO SI MIDOGO!!



Zilikuwa Siku, Wiki na sasa ni Miezi mitano tangu ulipozaliwa,
Mungu akupe uhai, ufike mbali ukubwani, Maisha ni Mitihani,
Hongera Fahim mwanangu, Miezi Mitano umeitimiza!

HAPA NDIPO ANAPOANDALIWA PWEZA?



Mkazi huyu wa jijini Dar es Salaam alikutwa na blogu hii akiandaa samaki aina ya pweza na ngisi kwenye mazingira machafu leo asubuhi, Soko la Samaki Magogoni (Feri). Maandalizi ya chakula kwenye mazingira ya aina hii ni hatari hasa ukuzingatia mtumiaji ni binadamu mimi na wewe.

Mamlaka zinazohusika na masuala ya usafi wa mazingira kwenye maeneo nyeti hasa Sokoni hazina budi kuchukua tahadhari kwa kufanya ziara za mara kwa mara maeneo hayo kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata taratibu na kanuni za usafi wakati wakiandaa bidhaa zao ili kuepusha maradhi ya milipuko kwa watumiaji.

Friday, August 6, 2010

WAZIRI LI DONGDONG WA CHINA ATEMBELEA TSN



Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya TSN inayochapisha magazeti ya Serikali ya Daily News na Habari Leo, Mkumbwa Ally (kushoto) akimtembeza mgeni wake, Naibu Waziri wa Uchapishaji na Habari wa China, Bi. Li Dongdong kuangalia shughuli za uzalishaji wa magazeti hayo ndani ya ofisi za Kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam leo asubuhi. [Picha: kwa hisani ya Yusuf Badi wa TSN]

SHEIN AFUNGUA UJENZI KITUO CHA AFYA BUMBWI SUDI



Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Wananchi wa kijiji cha Bumbwi Sudi kiliopo katika Wilaya ya Magharibi Unguja leo. jumla ya shilingi miloni 25.4 zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho. [Picha: Kwa hisani ya Amour Nassor wa VPO]

KITI CHA KWANZA CHA SPIKA WA BUNGE LA TANGANYIKA LA MWAKA 1962


Hiki ndo' kiti cha kwanza cha Spika wa Bunge ambacho kilitolewa kama zawadi na Bunge la  Uingereza (House of Common) kwa Bunge la Tanganyika mwaka 1962 mara baada ya Uhuru. Kiti hiki kimetumika nchini mpaka mwaka 2005. [Picha: kwa hisani ya Owen Mwandumbya wa Bunge].

Monday, August 2, 2010

MTIKILA AYEYA JELA MIEZI 6

Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha DP amedakwa leo na makachero waliokuwa wakimsaka muda mrefu huku wakiwa na 'kibali cha kumkamata' na kufikishwa Mahakama ya wilaya Ilala ambako alikuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita hapo awali.

Mtikila ambaye alionekana kutoamini jambo hilo huku akionekana mwenye kujiamini zaidi, alikuwa akidaiwa deni la zaidi ya shilingi milioni 9 na mkazi mmoja wa jijini hapa Dar es Salaam, Mama Pascazia Zelamula Matete (61) ambaye kitaaluma ni Mwalimu.

Kwa mujibu wa Mama Pascazia, alimkopesha fedha hizo ili ziweze kumsaidia kwenye biashara zake, lakini imekuwa ngumu kwa Mtikila kurudisha fedha hizo kiasi cha kumsababishia mama huyo kutengwa na familia yake hususan mumewe ambaye alimwambia atamrudia tu endapo atakuwa amerudishiwa fedha hizo.


Mtikila akiingia kwenye gari la Polisi kuelekea kituo cha Msimbazi leo

"Hata watoto wangu nao wamenitenga, sasa naishi maisha magumu, nimetengwa na mume wangu, watoto wangu sababu ya huruma yangu ya kumsaidia Mtikila. Leo siondoki hapa, nitafia hapahapa mpaka fedha zangu azirudishe." Alisema mama huyo.

Mtikila alichukuliwa na gari la Polisi wa Kituo cha Msimbazi na kupelekwa kituoni huko kwa ajili ya kuhifadhiwa bada ya muda wa mahakama kuwa umekwisha na anatarajiwa kupelekwa jela kwa kipindi cha miezi sita, jambo ambalo binafsi ameridhia.

Sunday, August 1, 2010

KURA ZA MAONI ZANOGA: MTEMVU AONGOZA KATA YA MTONI: JANGWANI NUSURA ZICHAPWE KAVUKAVU: KADI FEKI ZAKAMATWA

Zoezi la upigaji kura za maoni kwa wanachama wa CCM kwenye matawi mbalimbali jijini hapa limekuwa na sura mbalimbali ambapo Jimbo la Temeke, Mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo Abbas Mtemvu mpaka kufikia majira ya saa moja usiku alikuwa akiongoza kwa kura Kata ya Mtoni.

Vituko vilianza kuibuka kwenye matawi mbalimbali huku kukiwa na malalamiko kadhaa kwa wanachama kuzuiliwa kupiga kura kutokana na majina yao kutoorodheshwa kwenye rejista mpya. Tawi la Misewe, Darajani na Segerea yote yakiwa kwenye Jimbo la Segerea malalamiko yalikuwa ya aina hiyo.



Jangwani, vituko vya kubiduliwa biduliwa kwa masanduku ya kupigia kura vilileta sura tofauti kabisa. Sababu inadaiwa ni kuwa majina ya watu yalikutwa yamepewa tiki kwenye rejesta ya majina.

Halikadhalika, kwenye Tawi moja lililopo Magomeni, zaidi ya kadi 500 za CCM zilirudishwa na wanachama wake na kuchukua za CUF papo hapo kutokana na kutoridhishwa na mchakato mzima wa zoezi hilo.

Tutaendelea kuwaletea updates za matokeo... Endelea kuhabarika