Sunday, August 22, 2010

NA HII NDIYO ATHARI YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI, KIJANA ACHOMWA MOTO MPAKA KUFA KAMA MNYAMA VILE!

Kijana huyu anayesemekana kuwa mkazi wa Goba ambaye jina lake halikufahamika mara moja alikutwa akiteketea kwa moto eneo la Kimara Mwisho, Dar es Salaam jana baada ya watu wasio na huruma kumchoma moto wakimtuhumu kwa wizi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hili, kijana huyu alishambuliwa na vijana waendesha pikipiki maarufu Bodaboda baada ya kumtuhumu kuiba pikipiki la mmoja wa vijana hao ambapo walimkamata na kuanza kumshambulia kabla ya kumchoma moto hadi kufa kikatili.



Inadaiwa kuwa, kijana huyu ilikuja kufahamika baadaye kuwa hakuwa mwizi kama ilivyodhaniwa na waendesha pikipiki hao bali alifika hapo kwa mafundi akiwa na pikipiki yake kwa ajili ya kutengenezewa na ndipo alipoazima moja ya pikipiki zilizokuwa kwa fundi huyo kwa ajili ya kwenda kuchukulia mafuta kuja kuweka kwenye pikipiki yake.

"Alipokuwa akipita njiani mwenye pikipiki lake akamwona na kuwaambiza wenzake na kuanza kumfukuzia akidhani kaibiwa pikipiki lake hilo," Anasema shuhuda na kuendelea, "Alipofika Kimara Kona aliegesha na kwenda kituoni kuchukua mafuta. Wale jamaa walipofika eneo hilo hawakumuona na kuamua kurudi, lakini wakiwa njiani walimwona tena kijana yule akirudi na pikipiki hilo akiwa amebeba mafuta na ndipo walipomdhibiti na kisha kuanza kumshambulia, kiasha wakamwagia mafuta yake aliyokuwa amebeba na kumuwasha moto." Alisema

Katika hali ya kushangaza, wakati kijana yule akishambuliwa polisi walifika eneo hilo na kisha kuodnoka pasipo kuchukua hatua zozote. Ndipo baadaye polisi wa Mbezi wakiwa na Defender walipowasili hapo kijana wa watu akiwa tayari amekwisha teketea kwa moto.

Ndugu zake kijana huyo walipopata taarifa walifika eneo la tukio na kuthibitisha mwili wa ndugu yao, ambapo walisema kuwa kijana wao hakuwahi kuwa mwizi na yeye alikuwa akijishughulisha na shughuli zake maeneo ya huko Goba.



Hili ni tukio la kusikitisha. Vyombo mbalimbali vimekwishazuia watu kujichukulia sheria mkononi vikiwa na maana nzuri tu kwa jamii. Kama mtu anatiliwa shaka, vyombo vinavyohusika vipo na taarifa zitolewe huko wao watashughulikia. Wahenga wanasema kuwa 'majuto ni mjukuu.' Na hivi ndivyo waliohusika na kitendo cha kumchoma moto kijana huyu wanavyojutia nafsi zao kwa namna moja ama ingine.

Wananchi wenzangu, tuache kujichukulia sheria mkononi. Na hii ndiyo athari kubwa ya kufanya hivyo. Kwa yeyote aliyehusika kwa namna moja ama nyingine aidha kwa kumtupia jiwe kijana huyu au kwa kushabikia wakati kijana huyu akishambuliwa, ajue kabisa nafsi yake inamsuta na kwa Mungu atajibu dhambi zake hizi.

Lakini pia askari polisi ambao hawana weledi na taaluma ya kazi hiyo, hawatufai kwenye jamii. Kwa nini askari waliofika eneo la tukio wakati kijana huyu akishambuliwa wasichukue hatua za kudhibiti hali hiyo, badala yake kulipuuzia na kisha kuondoka zao, huku nyuma wakiacha kijana huyu akichomwa moto kama panya aliyefumaniwa akidokoa kipande cha nyama kwenye chungu.

Na hii ndiyo athari kubwa ya kujichukulia sheria mkononi!!

No comments:

Post a Comment