Tuesday, November 16, 2010

PINDA NDIYE WAZIRI MKUU


Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amemtangaza Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano iliyobaki.

Spika Makinda alimtaja Mheshimiwa Pinda kuwa Waziri Mkuu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kupitia waraka wake aliomuandikia spika huyo na kusomwa mbele ya wabunge wa bunge hilo leo jioni.

"Nachukua fursa hii kumtangaza Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania." Alisema spika Makinda wakati akisoma barua hiyo iliyotumwa kwake.

Monday, November 15, 2010

WANAJESHI WA UINGEREZA WATOA MAFUNZO YA KUPAMBANA NA MAHARAMIA KWA WANAJESHI WA TANZANIA

Askari wa Jeshi la wanamaji wa Uingereza wamo nchini kwa siku tano ambapo wataendesha mafunzo ya kijeshi kwa askari wa jeshi la wanamaji hapa nchini ya namna ya kupambana na maharamia.

Askari hao waliowasili kwenye Bandari ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kwa meli ya kivita ya HMS Montrose watakuwepo kwa siku tano kabla ya kuondoka, ambapo vikosi mbalimbali vya wanamaji wa Tanzania vitapewa mbinu na mafunzo ya namna ya kupambana na maharamia.

Wakiwa njiani kuja hapa nchini, askari hao wameweza kudhibiti maharamia wa somalia kwa kiwango kikubwa. Kamanda wa meli hiyo, Jonathan Lett anasema, "Tumeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa maharamia katika pwani ya Somalia." Alisema.



British Royal Navy soldier, Rob McMurrich with his General Purpose Machine Gun

Sunday, November 7, 2010

MAJERUHI CHENGE ATANGAZA KUGOMBEA USPIKA



Mbunge mteule wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ametangaza azma yake ya kugombea bafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Dar es Salaam.

Chenge ametangaza azma yake hiyo mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini alipofanya nao mkutano kwenye hoteli ya Courtyard, eneo la Upanga Sea view, majira ya saa sita mchana.

"Nimewaita hapa leo ndugu zangu kwa lengo moja tu la kutangaza azma yangu ya kugombea nafasi ya Uspika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili niweze kutibu majeraha makubwa yaliyoumiza Bunge, Taifa na wananchi wa chama changu (CCM). Mimi kama ilivyo kwa wengine ni miongoni mwa majeruhi wa uongozi, Kama bunge, hatuna budi kukabiliana nalo kwa nguvu kubwa." alisema na kuongeza,

"Bunge letu limekuwa na changamoto kubwa katika miaka mitano iliyopita. Viongozi ambao wajibu wetu ni kuonesha njia badala yake tumekuwa vinara wa uzushi, uongo, fitna na majungu. Mimi ni mwarobaini (dawa ya kutibu) wa majeraha hayo, ambaye naamini ni kiongozi bora na nina uwezo na nia thabiti." Alisema

Sunday, October 31, 2010

BURIANI ELVIS MUSIBA



Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA), Elvis Musiba amefariki dunia leo kwenye hospitali ya TMJ, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na ndugu wa familia hiyo, marehemu Musiba alikutwa na mauti hayo majira ya saa nne asubuhi hospitalini hapo kutokana na maradhi ya mguu yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

Marehemu Musiba alikuwa akisumbuliwa na maradhi hayo ambapo mwezi oktoba mwaka huu alipelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kabla ya kufikishwa hospitalini hapo Jumamosi ya wiki iliyopita kwa mujibu wa ndugu hao.

Taratibu za mazishi zinafanywa nyumbani kwa marehemu Mikocheni, Dar es Salaam.

Marehemu Musiba katika uhai wake aliwahi kuwa Mtunzi mashuhuri wa simulizi za riwaya ambazo ni pamoja na 'Kufa na Kupona, Kikomo, Kikosi cha Kisasi, Njama na Hujuma na nyinginezo ambapo pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali za wakurugenzi zikiwemo Sematel Ltd (DRC), Exclusive Lodges Resort Ltd, Kamati ya Mahesabu ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Akaunti ya Milenia (Tanzania) na Kituo cha Uwekezaji cha TIC.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali pema Peponi, Amina.

ZAIDI YA NUSU YA WATANZANIA WALIOJIANDIKISHA HAWAJAPIGA KURA, WAANGALIZI WA SADC WASEMA HALI NI MBAYA, WAIOMBA SERIKALI KUNUSURU

Zaidi ya nusu ya watanzania waliojiandikisha kwenye daftari la kupiga kura hawakujitokeza kwenye zoezi la upigaji kura lililofanyika leo, kwenye maeneo mbalimba ya nchi.


Wasimamizi wakisubiri wapigakura

Wilaya ya Mkuranga, zaidi ya vituo vitano mahudhurio yalikuwa hayafikii hata nusu ya malengo. Katika kituo cha Godown-3, idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa ni 465 lakini mpaka kufikia saa saba mchana ni wapigakura 122 tu ndiyo waliojitokeza kupiga kura.

Kwenye kituo cha Shule ya Msingi Kiguza, mategemeo yalikuwa ni wapigakura 254, lakini mpaka kufikia saa sita mchana ni wapigakura 111 tu ndiyo waliojitokeza kupiga kura, hata hivyo hakukuwa na dalili yoyote ya kufikia alau nusu ya malengo hayo kutokana na mahudhurio ya mtu mmoja mmoja zaidi ya hata robo saa.

"Labda watakuja baadaye, asubuhi kunzia saa moja mpaka saa tatu ilikuwepo misururu mirefu, lakini kama unavyoona sasa hivi tumejikalia tu tunasubiri labda watakuja kabla ya saa 10." Alisema Msimamizi wa Kituo hicho, Malik Mporau.


Mawakala wakihakiki karatasi za kura

Hali ilikuwa ni hivyo kwenye kituo cha Picha ya Ndege-3 safari hii ikiwa mbaya zaidi, ambapo katika wananchi 400 waliolengwa kupiga kura, waliojitokeza ni 80 tu mpaka kufikia saa saba na nusu.

Katika Kata ya Toangoma, Kigamboni kwenye kituo cha Kongowe C-4, malengo yalikuwa ni wapigakura 420, lakini idadi iliyojitokeza ni wapigakura 120 tu mpaka kufikia saa nane mchana. Halikadhalika kwenye Jimbo la Mbagala, Kituo cha Ofisi ya Tarafa-3, waliokuwa wameandikishwa kwenye daftari la kupigia kura walikuwa ni 449 lakini waliojitokeza kupigakura mpaka saa nane na robo (saa moja na nusu baadaye kufungwa kwa zoezi) mchana walikuwa ni 130.

Napo kwenye kituo cha Bustani 4, Kata ya Mtoni ni watu 490 walioandikishwa kwenye daftari la kupiga kura, lakini mpaka kufikia saa tisa ni wapigakura 150 tu ndiyo waliokuwa wamejitokeza kupiga kura, kwa mujibu wa Radhia Hassan.

Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), na wale wa kutoka Jumuiya ya Madola (Common Wealth) walionesha kushtushwa na hali hiyo na kuishauri Serikali kuliangalia hilo kwa kuwashawishi wananchi wake kujitokeza kupiga kura kwenye chaguzi zijazo.

Mmoja wa wakala wa uchaguzi aliyefahamika kwa jina la Suleiman Iddi alisema kuwa waangalizi hao walitoa ushauri huo baada ya kubaini kuwa hali haikuwa shwari.

Friday, October 29, 2010

SIGARA HATARI!



Ni dhambi kubwa kwa Mungu kwa mtu anayejitoa mwenyewe uhai wake kwa namna yeyote ile. Unapofanya jambo ambalo unafahamu kuwa mwisho wa siku litakutoa uhai, ni sawa na kujinyonga mwenyewe.

Pichani ni pakiti za sigara zenye onyo kali kwa wavutaji wake. Ajabu ni kwamba onyo hilo limechukua nafasi kubwa kuliko nembo yenyewe ya bidhaa hiyo. Je, kwa hali hii,ukifa nani wa kulaumiwa wakati ushapewa onyo tena kwa maandishi makubwa tu?

DINI-VIONGOZI WA DINI WAUSIA UCHAGUZI WA AMANI

Viongozi wa dini leo wamefanya ziara kwenye vyama mbalimbali vya siasa kuhimiza Uchaguzi wa amani nchini.

Wakiwa kwenye Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), viongozi hao wamesisitiza uchaguzi wa haki ili wananchi wawapate wale viongozi waliowachagua na si vinginevyo.



"Hata vitabu vya dini vinakemea dhuluma ya haki, kila mwana adamu ana haki ya kuchagua akipendacho." Alisema Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum.



Naye Askofu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini (TEC), Paul Rukoza amesema kuwa wananchi wanatakiwa kujifunza ustahamilivu wakati wakupokea matokeo. Amesema kuwa wakati wa kmapeni kila upande hujiamini kupita kawaida kutokana na maandalizi jambo ambalo mwisho wa siku huweza kuibua malumbano na machafuko na kuathiri mfumo wa maisha.

"Hata hivyo tunapenda kuviasa baadhi ya vyombo vya habari vyenye mitazamo hasi kuhusu mikutano yetu sisi viongozi wa dini." Alisema

BEACH ZETU CHAFU!!

Huu ni ufukwe na wala si dampo. Eneo hili ni maarufu sana hapa mjini ambalo mwisho wa wiki wananchi hupendelea kwenda kujipumzisha na wengine kuoga kwa ajili ya kupunguza joto la jiji hili.



Eneo hili ni Ufukwe wa Coco almaarufu 'Coco Beach'. Lakini mandhari inayoonekana hapa haivutii kutokana na taka bahari zilizolundikana.

Je, kwa hali hii kuna ulazima wa kuendelea kuwapigia kelele wawekezaji wa kigeni kuwa wanatunyima wazalendo fursa za kufanya biashara? Mfano ufukwe huu ungekuwa chini ya mwekezaji wa kigeni unadhani hali ingekuwaje?

Tufanye kazi watanzania wenzangu na tuache kubweteka kwani mafanikio hayaji kiurahisi rahisi tu!

MATUNDA BWERERE, WAPI VIWANDA?

Tanzania imejaaliwa kwa kuwa na ardhi yenye kukubali kila aina ya zao. Matunda ni miongoni mwa mazao yanayostawi vizuri kwenye ardhi ya nchi hii. Unapofika msimu wake, matunda huwa ni mengi sana kwenye masoko yetu 'local markets'.

Huruma huwa inanijia pale ninapoona matunda hayo yanapokuwa mengi kwenye masoko yetu na kukosa wanunuzi ambapo mwisho wa siku huwa yanaoza, kuharibika kabisa mikononi mwa wafanyabiashara.



Wapi viwanda vya usindikaji wa matunda haya? Wapi viwanda vya kutengeneza 'juisi' za matunda haya? Matunda kama Machungwa, Maembe, Mananasi na mengineyo?

Kwanini Kenya waweze, sisi tushindwe? Kwa nini? Mchawi ni nani? Ona pichani ndizi hizi mbivu kwenye Soko la Buguruni zilivyolundikana hapo chini zikitafuta wanunuzi!! Baada ya siku chache pita tena hapohapo sokoni utaona namna ndizi hizo zilivyo ozeana, kulaliana na kupondekapondeka!

Tuesday, September 14, 2010

WASAJILI WAPYA WA MAHAKAMA KUU WAAPISHWA LEO


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu (katikati mbele), Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Ardhi, Regina Rweyemamu (wa pili kulia) na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Wasajili wapya wa Mahakama Kuu Tanzania walioapishwa leo

KAMPENI DAR ZADORORA, MIKOANI MBELE KWA MBELE

Wakati kampeni za uchaguzi zikiwa zinapata hamasa zaidi huko mikoani, huku jijini Dar tunashuhudia zikiwa zimedorora.

Utafiti unaonesha kuwa wakazi wa jiji hili wamekuwa wakibanwa na majukumu yao binafsi zaidi ukilinganisha na maeneo ya mikoani ambako wengi wa wananchi wa huko wamekuwa wakiacha shughuli zao kwa muda na kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni.

Mbali na hilo, pia hamasa zaidi katika kampeni za awamu hii ipo mikoani zaidi kutokana na wagombea wengi kuwa wapya ambao wameonesha kuchuana zaidi ukilinganisha na awamu iliyopita.

KAMPENI PICHANI LEO:

JK: BUMBULI





SALMA KIKWETE: MUSOMA




JUMA DUNI HAJI WA CUF: SUMVE



DK BILAL: DODOMA


TICTS WATIMIZA MIAKA 10 YA MAFANIKIO

Kampuni ya kuhudumia makontena bandarini (TICTS) jana imetimiza miaka 10 tangu kuanza kutoa huduma zake hapa nchini huku ikiwa imebadilisha taswira ya awali iliyokuwepo kwenye bandari zetu nchini.



Waziri wa Miundombinu Dk Shukuru Kawambwa anasema kuwa hali ya upakuaji makontena kwenye bandari zetu kabla kampuni hiyo haijaanza kuendesha shughuli zake hapa nchini ilikuwa si yakuridhisha ukilinganisha na sasa. "Tunaiombea iendelee kuleta mabadiliko mpaka kufikia mwaka 2025." Alisema.

Katika kuhakikisha shughuli za upakuaji makontena kwenye bandari zetu zinaboreshwa, jana kampuni hii imezindua winchi mpya moja yenye kasi na uwezo wa kubeba makontena mawili kwa wakati mmoja na kufanya idadi ya winchi nne yaani 'cranes'.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TICTS, Neville Bissett amewaambia waandishi wa habari pamoja na wadau waliohudhuria hafla hiyo jana Dar es Salaam kuwa kampuni yake kwa kushirikiana na vitengo mbalimbali vinavyotoa huduma bandarini hapo ikiwemo TRA, inaendelea kuboresha utendaji kazi wake ili kumaliza kabisa tatizo la mlundikano wa makontena.



Amewatoa hofu wateja wanaotumia bandari hiyo na kuwahakikishia mabadiliko ya hali ya juu zaidi. "Tumeboresha shughuli zetu ukilinganisha na tulivyoanza. Uwezo wetu umekuwa mkubwa kwa kuongeza winchi mpya na za kisasa zaidi." Alisema.

Saturday, September 4, 2010

Thursday, September 2, 2010

HEALTHIER DISABILITIES


A doctor with an Indian Navy examines girl with a disability at Uhuru co-education recently. A girl is a deaf and eyes disability.

NYAMISATI NA HAZINA ILIYOFICHIKA

Nyamisati ni kijiji kilichopo kilometa 42 toka barabara kuu iendayo Lindi na Mtwara. Kijiji hiki kipo katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hili ni wa kabila la wandengereko. Kijiji hiki kipo ufukweni mwa delta ya mto Rufiji unaotiririsha maji yake kwenye bahari ya Hindi. Hivyo basi utagundua kuwa uvuvi kijijini hapo ni moja ya shughuli zinazofanywa na wakazi wa kijiji hicho.



Pia, aina ya samaki wanaovuliwa Nyamisati ni aghalabu sana kupatikana Dar es Salaam kutokana na sababu ya kijiografia ya eneo hilo. Kamba ni miongoni mwa bidha inayovuliwa kwa wingi na wavuvi, wakazi wa Nyamisati na kuwasafirisha maeneo jirani na sehemu hiyo, ikiwemo Dar es Salaam.

Kamba hawa wanaovuliwa Nyamisati ni wa aina mbili, kamba wadogo 'Prons' na kamba wakubwa 'Lobsters'. Lobster mmoja wakati mwingine hufikia mpaka kilo 4. Na hii ina maana kwamba hata uvuvi wake ni tofauti na kamba wadogo 'Pons'.

Kilichonistajabisha ni kwamba, mbali na kupatikana kwa wingi kwa bidhaa hiyo ya kamba eneo hilo la Nyamisati, bado kuna changamoto ya soko la kuhifadhia bidha hao. Hii inasababisha uvuvi wa kamba hao unaofanyika Nyamisati kuwa ni mdogo na wa kubahatisha ukilinganisha na sifa yake.

USAFIRI WA MAJINI
Mitumbwi na boti ni nyenzo muhimu za usafiri kwa wakazi waishio vijiji jirani vilivyopo ng'ambo na Nyamisati. Mbali na wakazi wa vijiji jirani na Nyamisati, bali pia hata wakazi waisho kisiwa cha Mafia pia hutumia Nyamisati kama bandari muhimu kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao na huduma nyinginezo.


Wakazi wa Nyamisati wakiwa na bidhaa zao wakisafiri kwa boti


Wakazi wa Nyamisati wakisafiri kwa boti

"Mwendo wa kutoka hapa mpaka Mafia ni kama masaa matatu mpaka mawili na nusu." Anasema mmoja wa wakazi wa Nyamisati.

Wednesday, August 25, 2010

JK, DK BILAL WACHANJA MBUGA KWA KASI

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete pamoja na Mgombea Mwenza, Dk. Gharib Bilal wanazidi kuchanja mbuga kwenye kampeni zao za kuomba kura.

Rais Kikwete yeye leo alikuwa Bukoba mjini mkoa wa Kagera akiomba kura wakati Dk. Bilal yeye yupo mkoani Lindi akisaka kura hizo.


Pichani: Rais Jakaya Kikwete akiwa Bukoba mjini leo


Pichani: Dk Gharib Bilal akisalimiana na wakazi wa kijiji cha Mkwajuni, Lindi Vijijini.


Pichani: Wakazi wa Kijiji cha Kilangala wakisikiliza jambo

MADEREVA WAZEMBE SASA KUDHIBITIWA NA TEKNOHAMA



Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema akionyesha mfano wa leseni mpya zilizo kwenye mfumo wa Teknohama zinazotarajiwa kutumiwa na madereva nchini, wakati akifungua semina ya siku mbili kwa Makamanda wa Mikoa na Makamanda wa vikosi vya usalama barabarani na watendaji wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuhusu mchakato wa namna ya utoaji wa leseni hizo mpya, Dar es Salaam leo. PICHA: Hassan Mndeme wa Jeshi la Polisi.

MABADILIKO YA TABIANCHI YAZIDI KULETA ATHARI DUNIANI

Wanaharakati wa masuala ya Mazingira duniani wanaendelea na kampeni yao ya utunzaji wa mazingira ili kuiepusha sayari hii tunayoishi kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.



Lakini hilo linatatizwa na kuongezeka kwa shughuli za kila siku za binadamu zinazochangia kuongezeka kwa athari hizi uniani. Shughuli hizi kama viwanda, ukataji miti na uchomaji misitu na nyinginezo ni sehemu tu ya zinazochangia kupoteza taswira sura ya dunia.

Monday, August 23, 2010

JK MBELE KWA MBELE MWANZA

Rais Jakaya Kikwete ameendelea kukusanya pointi muhimu kwa wananchi zitakazomwezesha kuchaguliwa tena kushika wadhifa huo kwa kuendelea na mikutano yake ya kampeni katika wilaya za Serengeti na Sengerema, baada ya kumaliza Mwanza mjini, mkoani humo.



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia wananchi katika kata ya Nyehunge jimbo la Buchosa, wilaya ya Sengerema  leo mchana.

Sunday, August 22, 2010

NA HII NDIYO ATHARI YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI, KIJANA ACHOMWA MOTO MPAKA KUFA KAMA MNYAMA VILE!

Kijana huyu anayesemekana kuwa mkazi wa Goba ambaye jina lake halikufahamika mara moja alikutwa akiteketea kwa moto eneo la Kimara Mwisho, Dar es Salaam jana baada ya watu wasio na huruma kumchoma moto wakimtuhumu kwa wizi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hili, kijana huyu alishambuliwa na vijana waendesha pikipiki maarufu Bodaboda baada ya kumtuhumu kuiba pikipiki la mmoja wa vijana hao ambapo walimkamata na kuanza kumshambulia kabla ya kumchoma moto hadi kufa kikatili.



Inadaiwa kuwa, kijana huyu ilikuja kufahamika baadaye kuwa hakuwa mwizi kama ilivyodhaniwa na waendesha pikipiki hao bali alifika hapo kwa mafundi akiwa na pikipiki yake kwa ajili ya kutengenezewa na ndipo alipoazima moja ya pikipiki zilizokuwa kwa fundi huyo kwa ajili ya kwenda kuchukulia mafuta kuja kuweka kwenye pikipiki yake.

"Alipokuwa akipita njiani mwenye pikipiki lake akamwona na kuwaambiza wenzake na kuanza kumfukuzia akidhani kaibiwa pikipiki lake hilo," Anasema shuhuda na kuendelea, "Alipofika Kimara Kona aliegesha na kwenda kituoni kuchukua mafuta. Wale jamaa walipofika eneo hilo hawakumuona na kuamua kurudi, lakini wakiwa njiani walimwona tena kijana yule akirudi na pikipiki hilo akiwa amebeba mafuta na ndipo walipomdhibiti na kisha kuanza kumshambulia, kiasha wakamwagia mafuta yake aliyokuwa amebeba na kumuwasha moto." Alisema

Katika hali ya kushangaza, wakati kijana yule akishambuliwa polisi walifika eneo hilo na kisha kuodnoka pasipo kuchukua hatua zozote. Ndipo baadaye polisi wa Mbezi wakiwa na Defender walipowasili hapo kijana wa watu akiwa tayari amekwisha teketea kwa moto.

Ndugu zake kijana huyo walipopata taarifa walifika eneo la tukio na kuthibitisha mwili wa ndugu yao, ambapo walisema kuwa kijana wao hakuwahi kuwa mwizi na yeye alikuwa akijishughulisha na shughuli zake maeneo ya huko Goba.



Hili ni tukio la kusikitisha. Vyombo mbalimbali vimekwishazuia watu kujichukulia sheria mkononi vikiwa na maana nzuri tu kwa jamii. Kama mtu anatiliwa shaka, vyombo vinavyohusika vipo na taarifa zitolewe huko wao watashughulikia. Wahenga wanasema kuwa 'majuto ni mjukuu.' Na hivi ndivyo waliohusika na kitendo cha kumchoma moto kijana huyu wanavyojutia nafsi zao kwa namna moja ama ingine.

Wananchi wenzangu, tuache kujichukulia sheria mkononi. Na hii ndiyo athari kubwa ya kufanya hivyo. Kwa yeyote aliyehusika kwa namna moja ama nyingine aidha kwa kumtupia jiwe kijana huyu au kwa kushabikia wakati kijana huyu akishambuliwa, ajue kabisa nafsi yake inamsuta na kwa Mungu atajibu dhambi zake hizi.

Lakini pia askari polisi ambao hawana weledi na taaluma ya kazi hiyo, hawatufai kwenye jamii. Kwa nini askari waliofika eneo la tukio wakati kijana huyu akishambuliwa wasichukue hatua za kudhibiti hali hiyo, badala yake kulipuuzia na kisha kuondoka zao, huku nyuma wakiacha kijana huyu akichomwa moto kama panya aliyefumaniwa akidokoa kipande cha nyama kwenye chungu.

Na hii ndiyo athari kubwa ya kujichukulia sheria mkononi!!

Monday, August 16, 2010

VODACOM ILIPOFUTURISHA KARIMJEE


Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Dietlof Mare (kulia) akikabidhi ndoo ya mafuta kwa waumini wa kiislam


Akinamama wa kiislam wakifuturu sambamba na Mkurugenzi wa Mahusiano na Vodacom Fouandation, Mwamvita Makamba


Walimu na wanafunzi wa madrasa wakiimba qasida kabla ya kufuturu


Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Dietlof Mare (katikati) akifuturu na waumini wa kiislam


Waumini wa kiislam wakisubiri kufuturu

Hafla hiyo ilifanyika jana jioni kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Issa bin Shaaban Simba na Shehe Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.

Friday, August 13, 2010

CHATU WA KEKO APATIKANA



Chatu aina ya Sebei au 'African Rock Python' mwenye uzito wa kilogramu 8, urefu wa futi 7 na umri wa miaka 6, aliyekuwa amepotea siku kumi zilizopita Wizara ya Maliasili na Utalii, amepatikana leo.

Chatu huyo ambaye alizua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wanaoishi kata ya Keko, jirani na wizarani hapo, alipatikana majira ya saa 6.30 mchana wa leo akiwa amejificha kwenye mazulia mabovu na majenereta, ndani ya eneo hilo la wizara.

Kwa mujibu wa watumishi wa wizarani hapo, chatu huyo alikuwa akikamata panya na kula kwa siku hizo kumi. Lakini pia wamesema hakuna madhara yoyote yaliyotokea.

CHATU PICHANI:



MIGIRO AMUHANI MAREHEMU MZEE KAWAWA



Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro (wa nne kulia) Pamoja na familia ya marehemu Rashid Mfaume Kawawa wakiomba dua katika kaburi baada ya kwenda kutoa pole kwa familia hiyo Madale, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Mke wa Marehemu, Asina Kawawa, Dada wa Marehemu Bi Amina, mtoto wa marehemu Vita Kawawa (wa pili kulia) na Shekhe Abubakar Alli (kulia ambaye ni Imam wa Msikiti wa Kawawa. Picha: Yusuf Badi

FUTARI YA MFUNGO WA RAMADHAN..



Waumini wa kiislamu wa Msikiti wa Al- Islaamiya, Mabibo, Dar es Salaam wakifuturu kama walivyokutwa jana kwenye msikiti huo. Waumini wa dini hiyo nchini na duniani wapo kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao ni moja kati ya nguzo tano za dini hiyo. Picha: Sponsor

MBIO ZA MWENGE TURIANI, MOROGORO



Mfanyabiashara wa mjini Turiani, Wilayani Mvomero, George Kiluwa (katikati) akipokea kiasi cha sh milioni 15 alizokopeshwa na Chama cha Akiba na Mikipo Tursaccos cha Turiani, kutoka kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Dk Nassoro Ally Matuzya (kulia) katika halfa ya kupitiwa na Mwenge wa Uhuru, mwishoni mwa wiki mjini humo. Picha: John Nditi

JK AFUNGUA KIKAO CHA NEC (CCM) LEO



Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, akifungua rasmi kikao cha kamati kuu ya CCM Taifa kilichokutana jana katika ukumbi wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Makao Makuu mjini Dodoma. Picha: Amour Nassor, Ikulu Zanzibar

MAZIWA HAYA NI HATARI KWA WATOTO!



Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo,(kushoto) akionesha kopo la maziwa aina ya NAN 2 kwa waandishi (hawapo pichani) ambayo ni bandia hayafai kwa matumizi ya watoto. Kulia ni Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula Raymond Wigenge. Picha: Yusuf Badi

Tuesday, August 10, 2010

RAMADHAN KAREEM KWA WAISLAM WOTE NCHINI...



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al Hajj Dk Amani Abeid Karume akitoa salamu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa wananchi na waumini wa Dini ya Kiislamu na kuwatakia mafanikio katika ibada hiyo. Picha: Ramadhan Othman wa Ikulu, Zanzibar

JK AZINDUA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA (DART) LEO



Rais Jakaya Kikwete (katikati) akipatiwa maelezo kuhusu ramani ya Miundombinu ya mfumo wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) na Mtendaji Mkuu wa Wakala hao Cosmas Takule (kulia) alipozindua Ujenzi wa Miundombinu hiyo, jana eneo la Kivukoni Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Celina Kombani (kushoto) na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, John McIntire

Photo Source: Sponsor