Monday, January 25, 2010

MAMIA KUMZIKA MTOTO WA CHIFU FUNDIKIRA KESHO MAKABURI YA MWANANYAMALA

Mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanatarajia kumsindikiza aliyekuwa Mtoto wa Chifu Fundikira, Swetu Fundikira aliyeuawa kwa kudaiwa kupigwa na wanajeshi wa (jwtz), katika safari yake ya mwisho makaburi ya Mwananyamala kesho jijini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaka wa Mrehemu, Ismail Fundikira, marehemu anatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Mwananyama saa tisa alasiri.


Marehemu Swetu enzi ya Uhai wake..

"Kwa sasa tunasubiri taratibu za 'postmortem' kumalizika pale Muhimbili National Hospital pamoja na kusubiri baadhi ya ndugu walio mbali kufika msibani." Alisema.

Hata hivyo Ismail amesema wao kama wanandugu wamejipanga kuhakikisha kesi inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya haki kutokana na uzito wa kesi yenyewe.

Marehemu Swetu ameacha Mke na watoto wawili Misuka na Syalo ambao wapo nchini Uingereza na Uholanzi
Marehemu Swetu alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi baada ya kushushiwa kipigo na Askari wawili wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) katika ugomvi wa barabarani, Mwananyamala, Dar es Salaam.


Marehemu Swetu na Mkewe enzi ya Uhai wake..

Hata hivyo wanajeshi hao walitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi ambao wanashikiliwa katika kituo cha Salender Bridge.
Askari hao, ambao ni mtu na mkewe kutoka kambi ya Lugalo, wanadaiwa kumuua kijana huyo, Swetu Fundikira baada ya kumpiga wakiwa na mwanajeshi mwingine mmoja katika ugomvi wa barabarani uliotokana na askari hao kudai kuwa walifanyiwa fujo na kutukanwa na gari ambalo Swetu na wenzake walikuwa wamepanda.

Kwa mujibu wa taarifa za watu walioshuhudia tukio hilo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Elias Kalinga zinasema marehemu alifariki juzi usiku katika Hospitali ya Muhimbili, kufuatia kipigo cha wanajeshi hao.

Habari kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo zinasema kuwa askari hao walimpiga kijana huyo juzi katika eneo la Kinondoni A kwa madai kuwa aliwachomekea na gari lake.

"Askari hao walimshusha kwenye gari eneo la Kinondoni A na kuanza kumshushia kipigo. Baada ya kumpiga walimchukua na kumwingiza ndani ya gari lao na kuondoka naye," alisema mmoja wa mashuhudua hao, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

No comments:

Post a Comment